WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali waweke utaratibu utakaoruhusu
huduma za afya kuendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo yao hata
kama zoezi la usafi la kila mwezi litakuwa linaendelea.
Serikali imeweka utaratibu wa
wananchi kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira siku ya
Jumamosi ya mwisho wa mwezi, zoezi ambalo linashirikisha watu wote
wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma nyingine zoezi linalofanyika
kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 4.00 asubuhi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Alhamisi, Mei 11, 2017) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mheshimiwa
Abdallah Ulega mbunge wa Mkuranga.
Mheshimiwa Ulega alitaka
kupata kauli ya Serikali kuhusu maeneo ya kutolea huduma mbalimbali
zikiwemo za afya ambayo hufungwa wakati wa zoezi la usafi linalofanyika
kila mwezi nchini, jambo linalosababisha kero kwa wagonjwa na wengine
wenye dharula.
Waziri Mkuu amesema “Hospitali
na maeneo mengine ya kutolea huduma za afya hayawezi kufungwa, viongozi
wa maeneo husika waweke utaratibu mzuri utakaoruhusu huduma hizo
ziendelee kutolewa bila ya kuathiri zoezi la usafi wa mazingira,”.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali imeagiza tani 131,000 za sukari ili kukabiliana na
upungufu uliopo nchini. Amesema Serikali iko macho na inajua maeneo
yanayohitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji.
“Mahitaji ya sukari nchini
kwa mwaka ni tani 420,000, ambapo tunazalisha tani 320,000, hivyo
tunaupungufu wa tani 100,000 hata hivyo tumeagiza tani 131,000 na tayari
tani 80,000 zimewasili nchini, ambapo kati yake tani 35,000 zimeingizwa
sokoni,” amesema.
Ametoa kauli hiyo wakati
akijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub aliyetaka
Serikali iwahakikishie wananchi upatikanaji wa sukari hususan katika
kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa
mwezi huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, MEI 11, 2017
No comments:
Post a Comment