Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za mitaa TAMISeMI akiwa katika picha ya pamoja na
Viongozi wa Serikali, Madaktari Bingwa, Viongozi wa Dini na Siasa katika
Hospitali ya Mvumi.
……………………………………………………………………………………….
Na Shanni Amanzi
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)Selemani Jafo amemtaka
Mkurugenzi wa Wilaya ya Chamwino Athuman Masasi kuhakikisha kuwa Mradi
wa maji wa kijiji cha Manzase unamalizika ifikapo mwishoni mwa mwezi
mei, mwaka huu.
Jafo ameyasema hayo alipokuwa
anafanya ziara yake katika hospitali ya Mvumi ambapo amezindua huduma ya
Hospitali Kimbizi inayohudumiwa na Madaktari Bingwa ambao watatoa
huduma ya kitabibu ndani ya siku tano kuanzia leo, tarehe 15 hadi Mei
19, 2017.
Madaktari hao bingwa watatibu
magonjwa ya ndani kwa watu wote, watoto, mifupa, masikio, pua na koo,
meno, upasuaji na magonjwa ya uzazi kwa upande wa akinamama.
Alisema katika sehemu mbalimbali
alizopita kumekuwa na changamoto ya kukosa huduma bora katika vituo vya
Afya kutokana na urasimu walionao Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa na kufanya Wananchi wengi wasio na uwezo wa kupata huduma hizo
katika kipindi cha nyuma na kwa kipindi hiki Serikali imeshatoa
ufumbuzi ambao Viongozi mnapaswa kuzitumia vyema pesa za Miradi ya Afya
kama Busket Fund katika kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi wote.
Aidha Jafo amewataka Wananchi
kushiriki kikamilifu katika kupata huduma hizo kutoka kwa Madaktari
bingwa waliotoka katika hospitali mbalimbali nchini kwani huduma hizo
zinapatikana kwa bei nafuu na kutoka kwa Madaktari bingwa wenye uzoefu
mkubwa na wa muda mrefu .
Amepongeza ushirikiano uliopo wa
Mganga Mkuu wa Dodoma Dk.James Kiologwe Mbunge wa Jimbo la Mtera, Mkuu
wa Wilaya ya Chamwino, wadau mbalimbali pamoja na Kanisa la Anglikana
kwa kuweza kuendesha zoezi hilo la huduma.
Akihitimisha hotuba yake iliyojaa
maelekezo ya Serikali, Jafo amesema baada ya zoezi hili kukamilika
ingependeza madaktari bingwa wote walioshiriki zoezi hili katika Wilaya
zote za Dodoma waje kujipongeza mjini Dodoma na kuwa mfano bora wa
kuigwa kwa kuwa zoezi hili ni zoezi la kwanza kufanyika nchini na likiwa
limefanyika mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment