Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema
marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, wanahusika na sakata
la mchanga wa madini (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.
Pia
amesema Mkapa na Kikwete hawawezi kukwepa lawama juu ya mchanga huo kwa
kuwa mikataba kati ya Serikali na wawekezaji wa migodi inayotajwa,
ilisainiwa kwa nyakati tofauti wakati wao wakiwa madarakani.
Kauli
hiyo aliitoa mjini Dodoma jana alipozungumza katika mkutano wa Baraza
Kuu la Chadema uliokutanisha wajumbe 332, kati ya 370 waliotakiwa
kuhudhuria.
“Kama
kuna kitu kinaangamiza nchi, ni pale unapomwambia mfalme umevaa suti
wakati unaona yuko uchi. Katika sakata hili la mchanga, sisi kama chama
cha siasa, tumekaa na wataalamu wetu na kukusanya taarifa kwa sababu
wengi wanalizungumzia kwa kauli tofauti,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kwanza
kabisa inabidi tuelewe kwamba mchanga wa madini umekuwa ukisafirishwa
kwenda nje ya nchi kutoka kwenye migodi yetu miwili ya Bulyanhulu
kuanzia mwaka 2001 na Buzwagi kuanzia mwaka 2008.
“Eleweni
kwamba leseni za kusafirisha mchanga kwenda nje zilitolewa na Serikali
hii hii ya CCM na katika mikataba hiyo, kunatambulika kuna madini
mengine mbali na dhahabu katika migodi hiyo.
“Pia
makontena ya madini yanapokuwa bandarini kabla ya kusafirishwa, watu wa
TRA, TMAA, lazima wahakiki makontena yenye mchango huo ili kujiridhisha
na kilichomo.
“Wakati
mikataba hii inasainiwa, Rais Dk. John Magufuli alikuwa kwenye Baraza
la Mawaziri na pia Mkapa na Kikwete, wanayajua haya kwa sababu mikataba
ilisainiwa wakati wao wakiwa madarakani kwa nyakati tofauti.
“Nasema
hivyo kwa sababu enzi za Mkapa, mikataba mingi ya madini ilisainiwa na
hata Kikwete alipokuwa Waziri wa Nishati, kuna mkataba aliusaini.
“Kibaya
zaidi, CCM wamekuwa wakitumia wingi wao vibaya bungeni kupitisha sheria
mbovu kwa sababu hata mwaka 1997, Bunge lilipitisha kwa siku moja
sheria mbili za madini chini ya hati ya dharura na mwaka 1998, Bunge
lilipitisha sheria nyingine ya madini inaweka utaratibu wa uchimbaji wa
madini na kuruhusu wawekezaji kutoa mrabaha wa asilimia tatu ingawa
baadaye mrabaha huo ulibadilishwa na kuwa asilimia nne, huku sheria hiyo
ikiruhusu mchanga usafirishwe kwenda nje ya nchi.
“Yaani,
hata mikataba yetu inaruhusu wawekezaji kupewa misamaha ya madini
wakati sheria haisemi hivyo. Kwa hiyo, kinachotokea sasa ni matokeo ya
CCM kutufikisha tulipofika.”
Kutokana
na hali hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, alisema kuna uwezekano mkubwa Kampuni ya Acacia inayomiliki
migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambako mchanga huo ulipatikana,
ikafungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa
Migogoro.
“Jana
nilikuwa nasoma Gazeti la Telegraph la Uingereza ambapo wanasema tatizo
sio wawekezaji bali ni Waafrika wanaoingia mikataba ya uwekezaji na
wanasema kwa mujibu wa mkataba wetu, mchanga sio mali ya Tanzania bali
ni mali ya wawekezaji.
“Kwa
hiyo, kinachoonekana sasa ni kwamba nchi inaingia katika mgogoro wa
kidiplomasia na wawekezaji na kama wakiamua kwenda mahakamani,
hatutashinda kesi kwa sababu mikataba tuliisaini vibaya.
“Kibaya zaidi, ni kwamba kesi haitakuwa Kisutu, Kinondoni, Mwanza au Kigoma, bali itafanyika huko huko kwao,” alisema.
Mbowe
ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kwa kuwa uwezo wa Tanzania ni
mdogo katika uwekezaji wa miradi mikubwa, Serikali inatakiwa kuwa makini
kwa sababu si kweli kwamba wawekezaji wote ni wezi na pia si kweli
kwamba wote ni waaminifu.
Akizungumzia
hali ya kisiasa, Mbowe alisema katika uzoefu wao kisiasa, Serikali ya
awamu ya tano ndiyo ngumu katika harakati zao kwa sababu Rais Magufuli
anakandamiza demokrasia.
Kwa
mujibu wa Mbowe, alisema serikalini kuna baadhi ya viongozi wanaamini
njia pekee ya kuwaweka madarakani ni kuvunja sheria na kuminya
demokrasia, jambo ambalo wamelivumilia kwa muda mrefu na kuwafanya
viongozi hao waamini Chadema ni waoga.
Alitoa
mfano wa matukio aliyosema ni uminywaji wa demokrasia nchini ikiwa ni
pamoja na kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa, kukamatwa kwa wanasiasa wa
upinzani na kufikishwa mahakamani bila sababu na kupotea kwa kada wa
Chadema, Ben Saanane.
“Awamu
hii ya tano ni ngumu sana kisiasa, lakini pia inatoa fursa kwetu kwa
sababu wananchi wana maisha magumu kweli kweli kuliko Serikali yoyote
katika nchi yetu.
“Rais
lazima ajue kwamba matendo yake yanaathiri Watanzania milioni 50 na
ajue sisi tunahitaji pia aliyeko madarakani alete amani kwa sababu nchi
ni yetu sote.
“Kwa
kifupi, nchi yetu kwa sasa haiko salama, kisiasa, kiuchumi na wala
kijamii, kwa sababu kila mmoja anashuhudia jinsi watu wanavyouawa Rufiji
na Mkuranga.
“Pamoja
na hayo, eleweni kwamba haki haipatikani kwa kuombwa bali kwa
mapambano. Kwa hiyo, lazima katika kikao chetu hiki tutoke na uamuzi
mgumu ili watawala wa nchi hii waelewe salama ya nchi ni kusimamia haki
kwa watu wote na sio kwa wana CCM peke yao, kama mbwai na iwe mbwai,” alisema Mbowe.
No comments:
Post a Comment