Watu
saba akiwamo ofisa wa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa,
Rwige Ogunya wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mwanza kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi baada ya kukutwa na mapipa 200
yenye ujazo wa lita 50,000 za kemikali bashirifu inayodhaniwa kuwa ni
ethyl alcohol.
Pamoja
na Ogunya, wengine waliosomewa shtaka namba 1/2018 la Uhujumu Uchumi ni
Mwita Ikohi, Cholla Maginga, Jamal Kulusanga na Eunice Mazinge ambao
kwa pamoja walidaiwa kukutwa wakisafirisha mapipa hayo kinyume cha
sheria.
Mbele
ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Gwaye Sumaye
mwendesha mashtaka wa Serikali, Seth Mkemwa alisema kosa hilo ni kinyume
cha kifungu cha 15 (ib) cha sheria namba tano ya mwaka 2015 ya
kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya pamoja na marekebisho yake ya
mwaka 2016, na mabadiliko madogo ya mwaka 2017.
Akisaidiana
na mwenzake, Gastus Namgoba, Mkemwa alimwambia Hakimu Sumaye
aliyesikiliza shauri hilo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Wilbert Chuma kuwa tukio hilo
lilitendeka Desemba 13, 2017 katika eneo la kivuko cha Kigongo wilayani
Misungwi mkoani Mwanza.
Katika
shtaka namba 2/2018 la uhujumu uchumi, washtakiwa Emmanuel Munis (38)
na Samwel Petro (28) wanakabiliwa na kesi ya kujihusisha na biashara
haramu ya kemikali bashirifu kinyume cha kifungu cha 15 (ib) cha Sheria
Namba Tano ya mwaka 2015 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016, na mabadiliko madogo ya mwaka
2017.
“Mnamo
Desemba 20, mwaka 2017 katika eneo la Kiseke ‘A’ wilaya ya Ilemela
mkoani Mwanza, washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa la kukutwa na lita
414 za kemikali bashirifu inayodhaniwa kuwa ni ethyl alcohol,” alidai
Mkemwa
Washtakiwa
hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa
kusikiliza mashauri hayo na walipelekwa mahabusu ya Gereza Kuu la Mkoa
wa Mwanza, Butimba hadi Januari 22, kesi zao zitakapotajwa tena
mahakamani hapo.
No comments:
Post a Comment