Serikali
imesitisha kwa muda usiojulikana shughuli za uchimbaji wa madini katika
mgodi wa dhahabu wa ZEM uliopo kijiji cha Nyasirori wilaya ya Butiama
mkoa wa Mara.
Imesema
imechukua uamuzi huo baada ya uongozi wa mgodi huo kushindwa kutekeleza
maagizo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya
wafanyakazi.
Uamuzi
wa kusitisha uchimbaji wa dhahabu katika mgodi huo umetolewa Januari
13, mwaka 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo baada ya
kufanya ziara mgodini hapo.
Akiwa
mgodini hapo, Nyongo aliutaka uongozi wa mgodi kumkutanisha na
wafanyakazi, hasa wachimbaji jambo ambalo lilishindikana baada ya
kuzungushwa maeneo mbalimbali bila kuona mfanyakazi yoyote.
“Mbona
muda unazidi kwenda hao wachimbaji hawafiki, hebu twendeni huko huko
(chini ya ardhi) nataka niongee nao nione kama mmetimiza maagizo ya
Serikali mliyopewa wiki mbili zilizopita," amesema Nyongo.
Baada
ya kufika eneo la uchimbaji, naibu waziri huyo aliombwa asubiri kwa
maelezo kuwa wachimbaji hao wameitwa, kujikuta akiganda kwa zaidi ya saa
moja.
Kufuatia
hali hiyo aliutaka uongozi wa mgodi kusitisha shughuli za uchimbaji
hadi hapo utakapotekeleza maagizo waliyopewa, kubainisha kuwa ingawa
Serikali inasisitiza uwekezaji haipo tayari kuona wananchi wake
wakinyanyasika.
Wakati
Nyongo akisema kwa mujibu wa taratibu na sheria, wachimbaji hao
wanapaswa kulipwa mshahara usiopungua Sh400,000, meneja rasilimali watu
wa mgodi huo, Luo Giriquam amesema hawakuwaficha wafanyakazi hao.
“Hatukuwaficha,
uongozi uliwatafuta bila mafanikio kwa vile walikuwa ndani ya shimo
wakiendelea na shughuli zao,” amesema na kuahidi kutekeleza maagizo ya
Serikali.
No comments:
Post a Comment