Wakati
Chadema ikijibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi kuhusu tuhuma za uvunjivu wa sheria ya vyama vya siasa na
maadili ya vyama hivyo, huenda chama hicho kikakabiliwa na mambo matatu
kama adhabu.
Chadema
iliwasilisha majibu ya maelezo kuhusu tuhuma hizo jana katika ofisi ya
msajili yakiwa ni ya pili baada ya yaliyowasilishwa awali kutomridhisha
msajili.
Awali,
Chadema ilitakiwa kutoa maelezo kwa kuvunja sheria kutokana na kufanya
maandamano Februari 16 baada ya mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa
ubunge wa Kinondoni uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es
Salaam.
Baada
ya kuwasilisha majibu hayo wiki iliyopita, msajili alieleza
kutoridhishwa na aliiandikia Chadema barua nyingine akitaka maelezo kuwa
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutamo huo wa kampeni
alitoa lugha za uchochezi.
Katika
barua zote mbili kwa Chadema, Jaji Mutungi amekitaka chama hicho kutoa
maelezo ni kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka sheria
ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama hiyo.
Kwa
mujibu wa kanuni za Oktoba Mosi, 2007 zilizosainiwa na Waziri Mkuu
wakati huo, Edward Lowassa kifungu cha 6(1)(c)(d) zinaeleza wajibu wa
msajili kwa vyama vya siasa.
Kifungu
6(1)(c) kinasema, “Kuzuia kitendo cha uvunjifu wa kanuni za maadili
kisiendelee na kukitaka chama au kumtaka kiongozi wa chama
kujirekebisha.”
Kifungu (d) kinasema, “Kutoa onyo la maandishi kwa chama au kiongozi wa chama husika.”
Kifungu
(6)(2) kinaeleza, “Iwapo baada ya kutolewa onyo la kwanza kwa mujibu wa
kanuni (1)(d), chama cha siasa kitaendelea au kiongozi ataendelea
kukiuka maadili hayo, msajili atakemea hadharani ukiukwaji huo wa
maadili.”
Hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yake, msajili ana uwezo wa kuzuia ruzuku na hata kukifuta chama cha siasa.
Katika
barua ya Chadema iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika
iliyowasilishwa jana kwenye ofisi ya msajili imeeleza masuala kadhaa
yaliyowapata ikiwamo ya viongozi wake kutekwa, kuteswa, kushambuliwa na
wengine kuuawa.
Chadema
katika hoja ya kwanza inamweleza Jaji Mutungi kwamba katika barua yake,
“Hujaeleza chanzo au sehemu ulipoyatoa maneno hayo na wala hujaeleza
kifaa au chombo cha habari kilichotumika kunukuu maneno hayo iwe rahisi
kwetu kutoa maelezo. Tuhuma zako hazina ushahidi wa aina yoyote
ulioambatanishwa katika barua yako.”
Pili,
Chadema inasema, Februari 27, Mbowe alihojiwa na Jeshi la Polisi katika
Kituo Kikuu cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuhusu kauli aliyoinukuu
Jaji Mutungi ambayo ni sehemu ya ushahidi mahakamani.
“Kwa
kuwa bado shauri hilo la jinai halijamalizika na wakati huohuo ofisi
yako inaendelea na uchunguzi wa kimaadili wa jambo hilohilo. Tunashauri
usubiri jambo hilo limalizike kwa upande wa jinai kwa sababu ni
ukiukwaji wa taratibu za kimahakama kwa mamlaka mbili tofauti
kushughulikia jambo moja na lenye maudhui yanayofanana na kwa mtu
yuleyule,” inasema Chadema.
Tatu,
chama hicho kinasema hata kama maneno aliyonukuu yalitamkwa na Mbowe
azingatie kuwa moja ya wajibu wa wanachama wa Chadema ambao umeainishwa
katika Katiba ibara ya 5.3.5 ambayo yamenukuliwa:
“Kuwa tayari kupambana na namna yoyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi.”
Chadema imesema Mbowe kama mwanachama hakukosea kitu chochote katika maneno hayo kwa kuwa lugha hiyo ni wajibu wa mwanachama.
Hoja
ya nne, Chadema inaeleza matukio kadhaa yaliyowafika viongozi wake
tangu utawala wa awamu ya tano ulipoingia madarakani Novemba 5,2015
ikibainisha ni; kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge Tundu Lissu, kupigwa
kwa silaha za jadi kwa aliyekuwa mwenyekiti Mkoa wa Mwanza, Alphonce
Mawazo Novemba 14, 2015 na kutekwa na kuumizwa kwa aliyekuwa mgombea
udiwani wa Buhangaza wilayani Muleba mkoani Kagera, Nelson Makoti.
Pia,
kutekwa, kuteswa hadi kuuawa kwa katibu wake wa Kata ya Hananasif,
Daniel John, Februari 11 na kushambuliwa kwa mapanga na shoka hadi
kuuawa diwani wa Namwawala wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Godfrey
Lwena.
No comments:
Post a Comment