Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kumsomea hukumu msanii Agnes Gerald
maarufu kama Masogange anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya
kwa sababu anaumwa, amewekewa dripu na hawezi kutembea.
Hukumu
hiyo ilitarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri mara
baada ya upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali,
Costantine Kakula kuwaita mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi ya
Masogange na kuufunga na mshtakiwa mwenyewe kujitetea.
Ilipofika
saa 3:46 asubuhi leo Jumatano Machi 21, 2018 kesi hiyo iliitwa kwa
Hakimu Mashauri na wakili wa Serikali, Adolf Mkini alieleza kuwa kesi
ilipangwa kwa ajili ya hukumu ila mshtakiwa Masogange anayewakilishwa na
wakili Ruben Simwanza hakuwapo.
Hata
hivyo, mdhamini wa Masogange ambaye hakutaja jina lake alisimama na
kuiambia mahakama kuwa Masogange hakufika mahakamani kwa sababu anaumwa
na akawasilisha nakala za vyeti vya hospitali mahakamani hapo.
Mdhamini huyo amedai kuwa Masogange amewekewa dripu na hawezi hata kutembea.
Kutokana
na hali hiyo Mkini ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya hukumu.
Hukumu itasomwa Aprili 3, 2018. Wakili mwingine anayemtetea Masogange
ni Nehemiah Nkoko.
Masogange wakati akijitetea katika kesi hiyo aliiomba mahakama imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.
Masogange
ambaye anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na
Oxazepam, katika utetezi wake amedai kuwa yeye hajawahi kutumia dawa za
kulevya hata siku moja.
Akijitetea Masogange meidai kuwa mbali ya kuwa msanii pia alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo.
Masogange
katika kesi hiyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika
maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za
kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).
Pia anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.
No comments:
Post a Comment