Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD)
ya Kaliua kuwakamata watu wawili kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo moja
kuchukua chupa 50 dawa za kuua wadudu katika zao la pamba na mwingne
kutumia mzani wa rula uliopigwa marufuku kwa kuwa inatumika kuwanyonya
wakulima.
Mwanri
alitoa agizo hilo jana katika maeneo mbalimbali Wilaya Kaliua Mwanri
wakati wa kampeni zake kuelimisha wakulima wa pamba mkoani humo juu ya
upuliziaji sahihi wa dawa za kuua wadudu katika zao hilo.
Katika
tukio la kwanza lilimhusisha Wakala wa Kampuni ya Kahama Cotton Company
Limited (KCCL) wa Kata za Seleli na Kona Nne Boniface Kibiru
anayetuhumiwa kuchukua dawa za kuua wadudu wa pamba bila kufuata sheria
na taratibu na hivyo kusababisha fujo kwa wakulima wa zao hilo kwa hofu
ya wadudu kuathiri mazao yao shambani kwa sababu ya kukosa dawa hizo.
“OCD
mtafute alipo mtuhumiwa huyo …kamata na mpeleke Mahakamani kwa tuhuma
za wizi kwa sababu ushahidi upo …wananchi na viongozi wa kijiji
wametueleza kuwa mhutumiwa alichukua chupa 50 za dudu ba jambo ambalo
lilisababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima wengi na kuathiri mazao yao
kwa sababu ya kuwachelewesha kupiga dawa za kuua wadudu wakati
wakisubiri muafaka” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema
chupa hizo 50 alizochukua mtuhumiwa zingeweza kunyunyuzia ekari 50 za
pamba, kwa hiyo kitendo hicho ni sawa na wizi na hivyo lazima apelekwe
Mahakamani ili akaeleze hizo chupa alikuwa anazipeleka wapi.
Naye
Mtendaji wa Kijiji(VEO) cha Mwendakulima Regina Kataka alisema tukio
hilo lilitokea baada ya kutoka kuchukua dawa hizo katika eneo la Seleli
alipokuwa ametumwa kuzifuata na ndipo baada ya kuzifikisha alichukua
chupa 50 bila kufuata utaratibu na kubakiza 150.
Alisema
kesho wakiwa wanatarajia kuanza kugawa dawa hizo kwa ajili ya kusaidia
wakulima ndipo walipogundua upungufu katika makasha na wakaamua kumhoji
naye akakiri kuchukua chupa hizo kwa matumizi ya mashamba yake.
VEO
alisema kitendo hicho kilichosababisha kuchelewesha zoezi la kuanza
ugawaji dawa kwa wakulima kilisababisha malalamiko na usumbufu kwa
wakulima na ndipo walipoitisha kikao na kuamua kumpa adhabu ambaye
baadaye aliikataa kuitekeleza.
Alisema kuwa Kijiji hicho kina wakulima 500 ambao wamelima ekari 920 katika eneo hilo.
Akiwakilisha
kero yake kwa Mkuu wa Mkoa Mwanakijiji wa Mwendakulima Manane Mwalemi
alimwomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora amchukulie hatua mtuhumiwa huyo baada
ya kuwasababishia usumbufu na athari kubwa katika zao lao la pamba baada
ya kuwafanya wachewe kunyunyuzia dawa na hivyo wadudu kuathiri mazao
yao.
Alisema
awali katika kikao chao kijiji cha kumhoji Mtuhumiwa na yeye kukiri
kutenda kosa hilo waliamua kumwadhibu kwa mujibu wa Sheria zao za
Sungusungu za kumtaka awalipe shilingi laki tatu au ng,ombe mmoja kwa
ajili ya usumbufu na hasara ambayo wamepata kutokana na ucheweleshaji
aliwasababishia, lakini baadae alikataa kutekeleza adhabu hiyo.
“Tumefurahi
sana Mkuu wa Mkoa kufika hapo utatusaidia kutatulia tatizo la dawa hapa
kwetu…tulimkamata Mwakilishi wa KCCL Bw. Boface Kubiru akiwa ameficha
dawa za kuua wadudu katika pamba chupa 50 ,huku sisi hatuna dawa na
tulikubaliana kumwadhibu kwa mujibu wa Sheria zetu za Sungusungu za
kumpiga Masumule ya kulipa shilingi laki tatu au atulipe ng’ombe mmoja
lakini alikataa…Mkuu Mkoa tunaomba utusaidie maana yeye ndiye
alisababisha tuchelewe kupiga dawa na wadudu wakaongeza na kuanza
kuharibu pamba yetu…tunaomba umsughulikie Mkuu” alisema Mwalemi.
Katika
hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya
hiyo (OCD) kumkamata mumiliki wa Duka la kununua mazao mbalimbali aina
ya karanga, mahindi na choroko linalojulikana kwa jina Kaliwa liliko
Kitongoji cha Mkuyuni cha Kijiji cha Limbulasiasa kwa tuhuma za kununua
mazao hayo kwa kutumia mzani wa rula uliopigwa marufuku kwa kuwa
inatumika kuwanyonya wakulima.
Mkuu
huyo wa Mkoa alichukua hatua hiyo baada ya kumkuta mfanyabiashara huyo
akiendelea kutumia mzani huo licha ya kupigwa marufuku muda mrefu na
Serikali kwa sababu umekuwa ukitumika kuwaibia wakulima.
Alimwagiza OCD kuhakikisha anakamata pia mzani wake na mhusika ili aweze kushitakiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora anaendelea na ziara yake katika maeneo mbalimbali ya
Mkoa huo ambayo yanayolima pamba kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima wa
zao hilo juu ya unyunyuziaji sahihi wa dawa za kuua wadudu.
Na Tiganya Vincent, Tabora
No comments:
Post a Comment