Serikali
imesema inaandaa utaratibu wa kuhakiki vyeti vya taaluma vinavyotolewa
na vyuo vya elimu ya juu vya ndani na nje ya nchi.
Wakati
hayo yakielezwa, watumishi wa umma 14,409 wamebainika kuwa na vyeti vya
kughushi huku 1,907 wakiwa hawajawasilisha vyeti kwa ajili ya
kuhakikiwa licha ya Serikali kutoa muda wa kutosha kwa watumishi hao
kuwasilisha vyeti vyao Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa ajili ya
uhakiki.
Hayo
yalielezwa jana na Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro wakati
akipokea taarifa ya sita na ya mwisho ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi
wa umma iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde.
Taarifa
iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano Ofisi ya Rais Utumishi,
inaeleza kuwa mbali na Serikali kuandaa utaratibu huo, watumishi
waliosoma vyuo vya nje ya nchi, watapaswa kuviwasilisha Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania (TCU) ili vihakikiwe kujiridhisha uhalali na wake.
Katika
taarifa hiyo, Dk Msonde amebainisha kuwa uhakiki wa vyeti kwa watumishi
wa umma ni vya ufaulu wa kidato cha nne, sita na ualimu.
Alisema
katika awamu ya sita watumishi 5,696 wamehakikiwa vyeti vyao, kati ya
hao 5,404 sawa na asilimia 94.82 wamebainika kuwa na vyeti halali na
watumishi 295 sawa na asilimia 5.518 wamebainika kuwa na vyeti vya
kughushi.
Alisema
watumishi wa umma 511,789 wamehakikiwa katika awamu zote sita za
uhakiki, kati ya hao watumishi 494,554 sawa na asilimia 96.71 vyeti vyao
vimebainika kuwa ni halali, 14,409 sawa na asilimia 2.82 wamebainika
kuwa na vyeti vya kughushi na watumishi 1,907 hawajawasilisha vyeti vyao
kwa ajili ya uhakiki.
Katika
taarifa hiyo, Dk Msonde alisema ofisi yake imebaini watumishi 71 majina
yao halisi waliyoajiriwa nayo ni tofauti na majina katika vyeti
walivyotumia kujipatia ajira katika utumishi wa umma.
Amebainisha
kuwa ofisi yake ilichukua hatua ya kuwahoji wahusika ambao walitoa
sababu mbalimbali zilizosababisha utofauti wa majina yao ikiwamo
kubadili dini na kusema hilo liko nje ya uwezo wa taasisi yake na
ameliwasilisha kwa katibu mkuu utumishi kwa ajili ya hatua stahiki.
Baada
ya kupokea taarifa hiyo, Dk Ndumbaro, alisema anaamini waajiri
wameshawaondoa katika orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali
watumishi wote waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi kuanzia awamu ya
kwanza hadi ya tano ya uhakiki, isipokuwa waliobainika kuwa na vyeti vya
kughushi katika awamu ya sita iliyotolewa jana.
Kuhusu watumishi 1,907 ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa wametenda kosa kwa kutotekeleza maagizo halali.
kuhusu
watumishi 71 ambao majina yao halisi ni tofauti na yaliyopo katika
vyeti vyao, katibu mkuu huyo alisema suala hilo litafanyiwa uchunguzi na
kutoa taarifa itakayotoa maoni na ushauri wa hatua za kuchukuliwa.
Watumishi
295 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi katika uhakiki wa awamu ya
sita iwapo hawataridhika na matokeo ya uhakiki wanapewa fursa ya kukata
rufaa hadi Machi 31, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment