Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kamati yake ya maudhui
inafuatilia mahojiano ya mwanamuziki Nasseb Abdul maarufu Diamond
aliyoyafanya katika kituo cha Redio cha Times jijini Dar es Salaam.
Ofisa
Mkuu Idara ya Utangazaji ya mamlaka hiyo, Andrew Kisaka amesema
wamechukua uamuzi huo kwa kuwa mahojiano hayo yamefanyika katika kituo
wanachokisimamia.
Katika
mahojiano hayo, Diamond alimjibu Naibu Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kutokana na Serikali kuzifungia
nyimbo 15 mwezi uliopita, zikiwemo mbili za mwanamuziki huyo.
Kisaka
amefafanua kuwa kiutaratibu wao wanaangalia zaidi chombo ambacho
wamekipa leseni na kwamba, masuala mengine yatashughulikiwa na mamlaka
nyingine.
Amesema
suala hilo kwa sasa linafanyiwa kazi na kamati ya maudhui na kuahidi
kulitolea ufafanuzi siku za hivi karibuni akiwataka wananchi kuwa na
subira.
Wakati
TCRA ikisema hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk
Harrison Mwakyembe amesema amesikitishwa na matamshi ya Diamond kuhusu
kufungiwa kwa nyimbo hizo aliyoyatoa katika kipindi hicho.
“Maamuzi
ya kuzifungia baadhi ya nyimbo za wasanii wawili kwa kukiuka maadili
yalifanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa Shonza
ambaye analaumiwa na Diamond,” amesema.
“Diamond
atambue kuwa Serikali ina taratibu zake na maamuzi ya naibu waziri ni
ya wizara. Kama vikao na wasanii tumefanya vingi sana, lakini Diamond
hakuwahi kuhudhuria vikao hivyo, si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao
cha peke yake.”
Amesisitiza,
“Sheria ni ya watu wote bila kujali umaarufu au nafasi ya mtu katika
jamii, hivyo msanii Diamond anapaswa kutii sheria na mamlaka
zilizowekwa.”
Dk
Mwakyembe ameeleza kuwa sio busara kwa Diamond kushindana na Serikali
na endapo ana ushauri wowote ni vyema akawasilisha kwa njia sahihi,
lakini si kumshambulia naibu waziri kwa dharau na kejeli kama
alivyofanya.
“Diamond
kwa mafanikio aliyoyapata katika muziki, anatarajiwa kuwa mfano bora
kwa wanamuziki wenzake. Napenda kuwakumbusha wasanii wote kwamba sanaa
ni kazi kama zilivyo kazi nyingine,” amesema.
“Pamoja
na kuwa na kipaji hicho, wasanii wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni
na miongozo inayosimamia tasnia ya sanaa kama ilivyo kwa tasnia
nyingine.”
No comments:
Post a Comment