Mmiliki
wa kampuni mbili za mabasi za HBS Express na Sabena, Sultan Ahmed
maarufu kama Chapa, amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni iliyotokea
kisogoni nyumbani kwake Sikonge mkoani Tabora jana.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wilbrod
Mutafungwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana mkoani humo.
Kamanda
Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea jana saa 2:30 asubuhi nyumbani
kwa marehemu na kwamba chanzo cha kujiua kwake huko hakijafahamika.
"Bado tunachunguza tukio hili, amejipiga risasi mdomoni, tunachunguza chanzo cha tukio hili," alisema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda Mutafungwa alisema marehemu Chapa pia alikuwa akimiliki kituo cha mafuta ya petroli wilayani Sikonge.
Chapa
anakuwa mfanyabiashara wa pili nchini kujiua kwa kujipiga risasi katika
kipindi cha mwaka mmoja baada ya Festo Msalia, muuza vinywaji kwa bei
ya jumla mkoani Dodoma, kujilipua Machi mwaka jana.
Msalia alijiua kwa kujipiga risasi kichwani baada ya kukamatwa na shehena kubwa ya viroba.
Aliyekuwa
Kamanda wa polisi mkoani humo wakati huo, Lazaro Mambosasa alisema
marehemu aliondoka nyumbani kwake kwa kutumia gari aina ya Toyota Prado
na kwenda kujipiga risasi katika eneo la Veyula, nje kidogo ya mji wa
Dodoma.
Mfanyabiashara hiyo alikamatwa na shehena ya viroba Machi 3, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment