KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

April 24, 2018

TANZANIA NA ISRAEL KUANGALIA NAMNA YA KUSHIRIKIANA KATIKA MASUALA YA UTOAJI HAKI

Tanzania na Israel zimekubaliana kwamba ,  mataifa hayo mawili yana mengi ya kujifunza baina  yao hususani katika  eneo la utoaji wa haki na usimamiaji wa sheria.

Hayo yamejiri jana ( jumatatu) wakati Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi,  alipokutana na kufanya mazungumzo  na  Waziri wa Sheria wa Israel Bi. Ayalet Shaked.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Jengo la   Mikutano la Kimataifa la Mwalimu Julius    Nyerere ( JNICC), viongozi hao walikubaliana kwamba kuna haja na umuhimu wa   Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Israel kukutana  kwa lengo la  kuainisha maeneo ambayo  Ofisi hizo mbili  zinaweza kushirikiana.

“  Nadhani  tuna mengi ya  kujifunza kutoka kwenu na halikadhalika nanyi kuna maeneo ambayo   mnaweza kujifunza  kutoka kwetu. Hivyo basi, ninaamini  kwamba pale itakapowezekana,  kuna umuhimu wa mimi kukutana na  mwenzangu ili tuweze kuangalia maeneo ya kipaumbele ambayo tunaweza kubadilishana uzoefu na kupanua wigo wa ushirikiano  baina ya  nchi zetu”, akasema Dk. Kilangi.

Akayataja maeneo ambayo  anaamini Tanzania na Israel  zinaweza kushirikiana  ni  pamoja na  namna  bora  ya  kuimarisha  mifumo ya utoaji  haki na  ushauri wa kisheria wenye tija, pamoja na eneo la uwezeshwji ( capacity  building).

 Mwanasheria Mkuu , Dk. Kilangi  ambaye alifuatana na  Naibu Mwanasheria Mkuu wa  Serikali  Bw, Edson Athnas  Makallo, aliyatumia mazungumzo  kati yake na   Waziri Shaked kuelezea baadhi ya  majukumu yake anayoyatekeleza  kama  Mshauri Mkuu wa Serikali katika   masuala yote yanayohusu sheria pamoja    muundo mpya wa Ofisi  ya Mwanasheria   Mkuu ambao umehusisha kuanzishwa  kwa Wakili Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake,   Waziri wa Sheria wa Israel, ambaye  Tanzania inakuwa nchi yake ya kwanza kutembelea Barani Afrika, pamoja na kukubaliana na wazo la Dk. Kilangi la kuangalia uwezekano wa  Wanasheria Wakuu kukutana  katika muda utakaopangwa. Amesema kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali   ni Ofisi nyeti na yenye hadhi ya  juu kabisa   katika nchi yoyote ile ikiwamo Israel.

Akaongeza kwamba, majukumu anayoyatekeleza Mwanasheria Mkuu wa  Serikali, Dk. Adelardus Kilangi  yanashabihiana  na  anayotekeleza  Mwanasheria Mkuu wa   Israel  yakiwamo ya kuisimamia  serikali katika  masuala yote yanayohusu sheria, kuiwakilisha serikali katika mahakama za juu na mahakama za chini pamoja na kuendesha mashauri  ya jinai  hivyo wawili  hao wakipata fursa ya kukutana bila shaka watakuwa na mengi ya  kujadiliana na  kushirikiana.

Waziri wa Sheria wa Israel Ayalet Shaked anaongoza ujumbe wa  wafanyabiashara kutoka Israel ambao upo hapa nchini  kukutana na  wafanyabiashara wa  Tanzania.

No comments:

Post a Comment