WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi,
Bibi. Pudencis Protas kumkamata Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC) wa wilaya ya Ruangwa Bw. Anthon Mandai kutokana na tuhuma
za matumizi mabaya ya madaraka.
Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa walimu wakimlalamikia kiongozi huyo kuwa na tabia za kudai rushwa, kutowapandisha madaraja, ulevi pamoja na kuwaita walimu hao kwenye vilabu vya pombe kwa ajili ya kuwasikiliza matatizo yao.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 12, 2018) wakati
akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa akiwa
katika siku ya mwisho ya ziara kyake ya kikazi wilayani hapa. Bw.
Mandai anakaimu nafasi hiyo tangu Juni, 2012.
Amesema
mbali na kulalamikiwa na walimu kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ulevi
na kuwaita walimu katika vilabu vya pombe pindi wanapohitaji
kuhudumiwa, pia amekuwa akighushi nyaraka za mirathi, jambo
linalosababisha baadhi ya familia za waliokuwa walimu kuchelewa kupata
haki zao.
“Huyu
Katibu ameshindwa kuwasaidia walimu katika kutatua changamoto zao na
badala yake amekuwa akitumia vibaya majina ya viongozi wakuu, ambapo
hata mimi alijaribu kutaka kunichakachua kwa kughushi muhtasari wa kikao
cha mirathi ya Mwalimu Suwedi Chikawe akitumia jina langu kuwa nilikuwa
mwenyekiti wa kikao hicho kilichokuwa na agenda ya kumbadilisha
msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa na familia jambo ambalo si la kweli,”
amesema.
Waziri
Mkuu amesema mbali na kukamatwa kwa Bw. Mandai, pia amemuagiza Kamanda
Pudencis afanye uchunguzi wa kina utakaowezesha kukamatwa kwa mtandao wa
watu wote wanashirikiana na kiongozi huyo katika kughushi nyaraka za
vikao vya mirathi.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wabadilike na
wafanye kazi kwa bidii, waachemazoea na watumie utalaamu wao vizuri
katika kuwahudumia wananchi na Serikali haitowavumilia wafanyakazi
watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao.
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi kuwachukulia hatua
watumishi wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu wanaitia
hasara halmashauri yao na Serikali kwa ujumla.
"Msimamo
wa Serikali ni kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo, hivyo
watumishi wajiepushe na vitendo vya rushwa na matumizi mbaya ya fedha za
umma."
Pia
Waziri Mkuu amewataka watendaji hao wawe na mpango wa kuwatembelea
wananchi katika maeneo yao hususan ya vijijini kwa ajili ya kusikiliza
kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU





No comments:
Post a Comment