Mwandishi wetu
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa udiwani katika
kata 37 za Tanzania Bara zilizopo katika Halmashauri 27 na mikoa 13 ya
Tanzania Bara, utakaofanyika tarehe 13 Oktoba mwaka huu.
Akitangaza
uchaguzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles
Kaijage, alisema fomu za uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo
zitatolewa kati ya tarehe 15 hadi 21 Septemba, mwaka huu.
Alisema
uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 21 Septemba, mwaka huu wakati
kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 22 Septemba hadi tarehe
12 Oktoba mwaka huu.
Jaji
Kaijage alifafanua kuwa uchaguzi huo unafuatia Tume kupokea taarifa ya
uwepo wa nafasi wazi za udiwani kwenye kata hizo kutoka kwa Waziri
mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kwa kutumia kifungu cha 13(1) cha
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.
“Baada
ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3)
cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Tume ina utaarifu umma
kuhusu kuwepo kwa Uchaguzi mdogo katika Kata hizo thelathini na saba
(37).”, alisema Jaji Kaijage.
Kufuatia
uchaguzi huo, Mwenyekiti huyo wa NEC alivialika Vyama vya Siasa, Wadau
wote wa Uchaguzi na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.
Aliongeza
kwa kuviasa Vyama vya Siasa na Wadau wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya
Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa (Madiwani), 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani ya mwaka 2015 na maelekezo yote yaliyotolewa au
yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi huo.
Wakati
huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Madiwani watatu Wanawake wa
Viti Maalum kujaza nafasi wazi za madiwani katika Halmashauri tatu za
Tanzania Bara.
Akitangaza
uteuzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles
Kaijage, aliwataja madiwani hao kuwa ni Halima Salum Kisenga (CCM) wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni.
Wengine
walioteuliwa ni Emmy Anania Shemweta kupitia CCM katika Halmashauri ya
Wilaya ya Lushoto na Nuru Mwalimu Chuma kupitia Chama cha Wananchi (CUF)
katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Jaji
Kaijage alisema uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka
kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye aliitarifu Tume
kuwepo kwa nafasi wazi kupitia vyama hivyo baada ya walioteuliwa
kufariki dunia na kujiuzulu.
No comments:
Post a Comment