Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa(pichani) amedai kuwa nchi inayumba kwa sababu Serikali inakumbatia wawekezaji wezi na wasiojali maslahi ya Watanzania.
Amesema hilo lilidhihirika wakati Rais Jakaya
Kikwete alipokuwa akilihutubia Taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dar es
Salaam, kwa kuwatetea wawekezaji huku akijua baadhi yao siyo waaminifu.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Tegeta katika
mkutano wa hadhara uliolenga kutatua kero za wakazi wa Tegeta Magereji,
Dk Slaa alisema: “Hata wakazi wa Magereji mnataka kuhamishwa kutoka eneo
lenu la biashara na mwekezaji ambaye tulimtaja katika orodha ya
mafisadi wa nchi hii mara nyingi tu. Rais Kikwete anatakiwa kutambua
kuwa Watanzania wamewachoka wawekezaji wezi, tunataka wawekezaji
watakaowanufaisha wananchi.”
Alisema zaidi ya Sh1 trilioni za Meremeta,
Richmond na Escrow zimeibwa na wawekezaji. “Nchi haiwezi kutafunwa kila
siku halafu sisi tunakaa kimya. Haki inaweza kucheleweshwa tu, lakini
itapatikana.”
Kuhusu mgogoro wa eneo hilo la Tegeta Magereji, Dk
Slaa alisema Chadema wataweka mawakili wao atakayeshirikiana na wa
upande wa walalamikaji, kwa lengo la kuhakikisha wananchi hao wanapata
haki yao.
Mgogoro wa Mtaa wa Magereji ulianza takribani
miaka mitano iliyopita baada ya mafundi magari waliohamishwa na Manispaa
ya Kinondoni kupelekwa eneo hilo na baadaye kutakiwa kuhama kwa madai
kuwa eneo hilo limechukuliwa na wawekezaji.
Katika mkutano huo alikuwapo pia mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Madale kwa tiketi ya CCM, Gratian Mbelwa ambaye
aliungana na Chadema kukemea dhuruma wanayotaka kufanyiwa wananchi hao
na Serikali huku akidai kuwa inachochewa na baadhi ya watendaji wa
Serikali Kuu.
Mbelwa alisema wakazi hao wamewekeza zaidi ya Sh35
bilioni katika eneo hilo, lakini wanatakiwa kulipwa fidia ya mifuko 10
ya saruji kila mmoja jambo lililoelezwa kuwa ni sawa dhuluma. Eneo hilo
lina watu 4,000.
Huku akiwa amevalia sare za CCM, Mbelwa alisema
mgogoro wa Tegeta Magereji ni sawa na Tegeta Escrow nyingine, kauli
iliyowafanya wananchi wamshangilie.
Mbelwa alisema mpaka sasa wananchi wamechangishana zaidi ya Sh70 milioni kwa ajili ya kuendesha kesi hiyo.
Katika mkutano huo, Dk Slaa alijibu maswali matano
kutoka kwa wananchi huku akimtupia lawama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Jordan Rugimbana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaamm Saidi Meck Sadiki kwa
kuulea mgogoro huo.
Alisema hata Rais Kikwete anaujua mgogoro huo kwa
muda mrefu, lakini ameamua kukaa kimya bila kuuzungumzia kila
anapozungumzia migogoro iliyoko nchini.CREDIT MWANANCHI
No comments:
Post a Comment