
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
Na Nathaniel Limu, Singida
JESHI la polisi mkoa wa Singida linamshikilia mkulima na mkazi wa
Matele-Kasulu mkoani Kigoma,Discon Bavumbi Masombo Kiyungu (45) kwa
tuhuma ya kumiliki risasi 271 za bunduki ya kijeshi aina ya SMG kinyume
na sheria.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka,
alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa Januari 18 mwaka huu huko Majengo
Manyoni mjini.
Alisema mafanikio hayo ya kumkamata mtuhumiwa yametokana na taarifa
sahihi zilizotolewa na raia wema kuwa mtuhumiwa alikuwa akisafirisha
risasi hizo kutoka Singida mjini na kuzipeleka Manyoni mjini.
Kamanda huyo alisema baada ya taarifa hiyo,askari polisi waliweka
mtego katika kituo cha mabasi kilichopo Majengo mjini Manyoni na
kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa baada ya kushuka kwenye gari aina ya
noah.
“Baada ya kukamatwa na kupekuliwa,aliweza kupatikana na risasi hizo
ambazo alikuwa amezificha ndani ya sanduku (briefcase) lake”,alisema.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni jangili na
husafirisha risasi kutoka nchi jirani ya Burundi na kuzipeleka porini
kwa ajili ya kuwindia Tembo.
Imebainika pia kuwa mtuhumiwa alikuwa na wenzake ambao hawakuweza
kubainika kwa majina na makazi waliofika katika kituo hicho cha mabasi
kwa ajili ya kumpokea lakini walipobaini kuwa mwenzao
amekamatwa,walitoroka na kukimbilia kusiko julikana.
Kamanda Sedoyeka alisema kuwa mtuhumiwa huyo bado anaendelea kuhojiwa
ili kujua mahali ilipo bunduki ambayo hutumia risasi hizo ikiwa ni
pamoja na kujua mtandao mzima wa ujangiri na kuwatafuta watuhumiwa
waliotoroka kwa lengo la kuharibu na kukomesha vitendo hivyo ambavyo
vinaharibu rasilimali ya taifa.


No comments:
Post a Comment