![]() |
| Mh. Zitto Kabwe |
Zitto aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alitimuliwa kwenye chama hicho hivi
karibuni na siku chache baadaye, akaibukia kwenye chama hicho na
kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu Taifa wa chama hicho.
Baada ya uchaguzi huo, Machi 29, 2015, ACT kilizinduliwa rasmi katika
hafla kubwa iliyoacha gumzo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond
Jubilee jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha watu mbalimbali kutoka
mikoa kadhaa ya Tanzania sambamba na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi.
Jeuri ya fedha iliyotumika kwenye uchaguzi huo, kwa kukodi ukumbi wa
gharama, kuwagharamia wajumbe wote kutoka mikoani na kurusha matangazo
ya runinga moja kwa moja kupitia runinga za ITV na Azam TV, ilisababisha
minong’ono mingi kuanza kusambaa kwamba nyuma ya chama hicho, kulikuwa
na mkono wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Haiwezekani chama ndiyo kwanza kimeanzishwa juzijuzi tu halafu wawe
na jeuri ya fedha kiasi hiki, kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye
runinga mbili za ITV na Azam TV kunagharimu fedha nyingi sana, Zitto na
wenzake wamepata wapi fedha hizo? Kuna mkono wa mtu hapa,” mdau mmoja
aliyeomba hifadhi ya jina lake, aliliambia Uwazi Mizengwe nje ya ukumbi
huo wakati uzinduzi ukiendelea.
Wasomaji wengine waliofuatilia uzinduzi huo, walipiga simu chumba cha
habari na kudai kuwa kuna zengwe limeandaliwa kumpaisha Zitto na chama
chake kwa lengo la kupunguza kura za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
katika uchaguzi mkuu ujao.
“Hawa jamaa (CCM) ni wajanja sana, wameamua kuwekeza ACT kwa kuwapa
fedha na kuwagharamia kila kitu ili kuwachanganya wapinzani. Unajua
mpaka sasa tayari kuna watu walikuwa Ukawa wameshahamia kwa Zitto, CCM
wamefanya makusudi ili waendelee kutawala, wanatumia ile falsafa isemayo
‘Divide and Rule’ (Gawanya kisha Tawala),” alisema Sunday Makweta
wakati akizungumza na gazeti hili.
Ili kupata ukweli wa zengwe hilo, Uwazi Mizengwe liliingia kazini
ambapo lilianza kwa kumtafuta Zitto. Alipopatikana, alisomewa madai
kwamba chama chake kinadaiwa kufadhiliwa na CCM kwa lengo la kudhoofisha
Ukawa ambapo alishangaa madai hayo na kufunguka:
“Huyo anayetuhumu hivyo aseme huyo mfadhili ni nani na kafadhili
nini. Yeyote mwenye mawazo hayo hafikirii. Wanachama wamejitolea,
gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja tumepewa discounts
(punguzo la bei). Tumechanga kutoka kwa marafiki, hiki chama ni sawa na
moto wa pumba, ni chama kikubwa na tumedhamiria.”
Uwazi Mizengwe lilimtafuta pia mwenyekiti wa chama hicho (Taifa),
Annastazia Mghwira alisema si kweli kwamba chama chao kinafadhiliwa na
CCM kwa sababu kwanza wana kesi dhidi ya chama hicho mahakamani kutokana
na madai ya kuibiwa kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Chama chetu kinapaa kutokana na wanachama kujitolea na tunataka kuhamisha uwezo kwa wananchi na kuing’oa CCM madarakani.”



No comments:
Post a Comment