KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

May 26, 2015

UTAMADUNI ULIVYOKOMBOA, KUTENGENEZA SURA YA AFRIKA

unnamed
Benjamin Sawe Katika kila jamii kuna shughuli na tabia ambazo huwatambulisha wao kama jamii fulani. Kwa mfano; ufugaji wa ng’ombe kwa jamii ya Wamasai au uvaaji wa hijabu katika jamii za Kiislamu kama Zanzibar ni mambo yanayozitambulisha kwa uharaka jamii hizo. Kwa msingi huo, utamaduni ni jinsi au namna watu wa mila fulani wanavyoishi kulingana na mila na desturi zao, tabia na shughuli zao za kiuchumi au zisizo za kiuchumi. Vilevile utamaduni unahusisha sanaa ambazo hutambulisha taasisi au jamii fulani. Kwa mfano, Wamakonde na uchongaji wa vinyago na ngoma yao Sindimba ama Wamasai kwa ufundi wa kusuka nywele aina ya sangita kama si mavazi yao aina ya lubega huku wakiwa wamening’iniza sime kiunoni. Katika karne ya 20 utamaduni ulimwenguni ulikua na kuwa kama nyanja muhimu katika elimu ya asili ya binadamu kuhusiana na mambo yote ambayo sio matokeo ya kijinsia. Nchini Marekani, elimu hii humaanisha uwezo wa binadamu kutambua na kuonesha tabia za kibinadamu na ubunifu katika kufanya vitu mbalimbali kwenye jamii na jinsi watu wanavyoishi sehemu mbalimbali ulimwenguni. Barani Afrika kulikuwa na tamaduni ambazo watu walikuwa nazo kabla ya kuja kwa wakoloni katika karne 19 na zimeendelea kudumu hadi leo. Waafrika wamekuwa wakitumia tamaduni zao kama njia ya maisha yao ya kila siku kupitia sanaa, ubunifu, ufundi na ujuzi mwingine katika kuendesha maisha yao. Hata hivyo, baada ya kuja kwa wakoloni utamaduni wa Kiafrika uliharibiwa na kuvurugwa kwa kiasi fulani. Wakoloni walipuuza tamaduni za Waafrika na kuingiza tamaduni zao. Walipuuza tamaduni kama jando na unyago, michoro ya asili na viwanda vidogo vidogo vya mikono. Badala yake wakaingiza tamaduni zao kama staili za kuvaa za kizungu, dini, elimu ya kikoloni na sanaa zao. Hii yote ni kwa sababu wakoloni lengo lao kubwa ilikuwa ni kuwaibia Waafrika rasilimali zao. Lakini Waafrika waliendelea kufanya tamaduni zao kwa siri na kuzihifadhi na kwa sehemu kubwa walitumia utamaduni zao kama chombo cha ukombozi. Katika Tanganyika waliibuka wasanii wengi ambao walitumia sanaa zao kuweka uzalendo na kuleta ukombozi katika nchi yao. Mfano mzuri ni Shaaban Robert ambaye alikuwa mtunzi wa mashairi na mwandishi wa riwaya. Mtu huyu ana mchango mkubwa, si katika kuhamasisha ukombozi pekee, bali pia katika Lugha ya Kiswahili kwa sababu kazi zake zinatumika kwenye fasihi ya Kiswahili mashuleni na sehemu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment