Baraza la Ulamaa limemchagua, Sheikh Abubakar bin Zubeir Ally, kuwa Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania katika kikao chake kilichofanyika jana mjini Bagamoyo, mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila, Kaimu Mufti Zubeir alichaguliwa kwa
kura za wajumbe wote wa baraza hilo.
“Kaimu Mufti amechaguliwa leo (jana) asubuhi na Baraza la Ulamaa
linaloundwa na wajumbe saba katibu naye akishiriki amepata kura nane
zilizompa ushindi,” alisema Sheikh Lolila.
Aidha, alisema baada ya kumchagua kaimu mufti huyo kitakachofuata
ni kutengeneza mikakati ya kufanya uchaguzi mkuu wa Bakwata baada siku
90 ambao utashirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa baraza hilo.
Alisema mkutano huo mkuu ndiyo utakaomchagua Mufti Mkuu mpya
ataziba nafasi ya Sheikh Mkuu Mufti, Issa Shabani Simba, aliyefariki
dunia Juni 15, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.
MATARAJIO YAKE
Kwa upande wake, Kaimu Mufti Mkuu, Sheikh Zubeir bin Ally, alisema
matarajio yake ni kuendeleza mambo aliyoacha Marehemu Mufti Simba.
“Matarajio yangu ni kuendeleza yote aliyofanya na aliyoacha Mufti Simba ikiwa pamoja na kuanzisha mapya,” alisema Sheikh Ally.
Kaimu Mufti Ally alisema katika kipindi chake cha kukaimu atajenga
mshikamano kati ya waislamu pamoja na kushirikiana na viongozi wa Baraza
la Ulamaa kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha uhai wa baraza hilo.
Alisema atakuwa tayari kupokea ushauri utakaosaidia kuijenga
Bakwata na kwamba ni matarajio yake ni kuifanyia marekebisho Katiba ya
baraza hilo iliyokuwa ikilalamikiwa muda mrefu kwa kushirikiana wajumbe,
katibu na watendaji ili iweze kukidhi matakwa ya Waislamu wote.
Aliwataka waumaini wa dini ya Kiislam na jamii kwa ujumla kuendelea
kulinda na kudumisha amani ili nchi iendeelee kuwa mahali pazuri na
salama kuishi na watu kuabudu.
DK. SLAA AMTEMBELEA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibroad Slaa, amemtembelea nyumbani kwake Kaimu Sheikh Mkuu, Mufti
Abubakar bin Zubeir Ally, kumpongeza na kumtakia majukumu mema
akimhakikishia ushirikiano kama jirani na kiongozi.
Sheikh Zuber atakaimu nafasi hiyo ya juu kwa siku 90 hadi hapo
atakapochaguliwa Mufti Mkuu kwa mujibu wa katiba ya Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata).
Zubeir anaishi mtaa wa Ufipa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, jirani na zilipo ofisi za Makao Makuu ya Chadema.
Mbali ya kumtakia kila la heri, Dk. Slaa alimuahidi Mufti Sheikh
Zuberi kuwa Chadema iko tayari wakati wowote kutoa ushirikiano
atakaouhitaji katika kutimiza wajibu wake huo.
“Nitumie fursa hii pia kusema tukiwa majirani zako hapa Mtaa wa
Ufipa, tukiwa viongozi ambao tunao wanachama, wapenzi na wafuasi wetu
wenye dini tofauti wakiwamo Waislam, naomba kukuhakikishia ushirikiano
kutoka kwetu wakati wowote katika kutimiza majukumu yako haya makubwa na
nyeti,” alisema. Mufti Simba alizikwa Juni 16, mwaka huu katika
makaburi ya Nguzo Nane, mkoani Shinyanga, mazishi yake yakiongozwa na
Rais Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa mamia ya wananchi wakiwamo viongozi
wa serikali, dini na vyama vya siasa.
Sheikh Mkuu mpya wa Tanzania atapatikana miongoni mwa wajumbe wa
Baraza la Ulamaa linaundwa na Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi na
naibu wake Sheikh Ali Muhidin Mkoyogole.
Wengine ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Fereji, Sheikh wa Mkoa
wa Shinyanga, Ismail Makusanya, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa
na Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Masoud Jongo.



No comments:
Post a Comment