![]() |
| Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa tahadhari kwa wagombea watakaokiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 watakuwa wanajiweka katika hatari ya kutoteuliwa na vyama vyao.
Hadi sasa vyama ambavyo makada wake wameanza kuchukua fomu za
kuomba kuwania urais ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi
(CUF).
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (pichani), alitoa
tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi na sheria ya vyama vya
siasa ambazo zinapaswa kuzingatiwa na vyama na wanasiasa katika kipindi
hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
“Natoa tahadhari au angalizo kwa vyama vya siasa na wanasiasa
wasipuuzie utii wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa sababu kutawaathiri
nje na ndani ya vyama ,” alisema.
Mutungi alisema katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mgombea
yeyote au chama cha siasa asipozingatia sheria hiyo atakuwa anahatarisha
nafasi yake ya kugombea na kutoteuliwa na chama chake kutokana na
kukiuka masharti yaliyopo ndani ya sheria hiyo.
Alisema chama cha siasa kitakachopuuzia sheria ya uchaguzi na
kikapitisha mgombea ambaye amekiuka masharti yaliyomo ndani ya sheria
hiyo kitakuwa kinapitisha mgombea ambaye atawekewa pingamizi na atakuwa
amejiharibia nafasi hiyo.
“Sitaki kuamini kuwa sekretarieti ya chama kilichosajiliwa
kisizingatie utii wa sheria ya uchaguzi, kila mtu ni jukumu lake
kuzingatia utii wa sehria bila shututi,” alisema.
Jaji Mutungi alisema kipindi hiki siyo muda mwafaka wa kufanya
tathmini kama vyama vya siasa na wagombea wamezingatia sheria hiyo kwani
hivi sasa ofisi ya msajili na vyombo vingine vinaendelea kufuatilia
suala hilo na muda ukifika matokeo yatatolewa kwa kuweka wazi vyama na
wagombea waliokiuka sheria.
Aliongeza kuwa sheria ya gharama za uchaguzi madhumuni yake
yaliwekwa kwa misingi ya kutaka kudhibiti matumizi ya gharama katika
mchakato wa uchaguzi na kuthibiti vitendo vinavyokataza na sheria ya
nchi.
“Vyama vya siasa vinapaswa kufahamu kuna mambo ambayo sheria
inakataza ikiwamo kufanya malipo kwa wapigakura ili kumchagua mgombea
fulani, kuahidi kazi ama cheo, kutoa mikopo na ahadi ama makubaliano
yoyote kwa mpiga kura ili kumchagua mgombea,” alisema.
Sheria ya gharama za uchaguzi imeainisha wazi kuwa chama cha siasa
ndicho kitagharamia mchakato wa kura ya maoni na kampeni za uchaguzi
ikiwa ni pamoja na gharama zote zitakazotumika kwa ajili ya
uhamasisahaji kwa lengo la kumnadi mgombea kwa wapiga kura.
Pia sheria hiyo inaelekeza kuwapo kwa uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea wao kabla na baada ya uchaguzi.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari
2010.
CHANZO:
NIPASHE
|
June 17, 2015
MSAJILI WA VYAMA AONYA MATUMIZI MAKUBWA KAMPENI ZA UCHAGUZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment