![]() |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
akizungumza na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba bungeni mjini
Dodoma jana. Picha na Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma. Harakati za wagombea urais wa Jamhuri
ya Muungano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana zilihamia katika
ukumbi wa Bunge ambapo kila mmoja wao alikuwa akitafuta mbinu za
kusalimiana na wabunge.
Hata hivyo baadhi ya wagombea hao walikuwa
wanatumia nafasi hiyo kuzunguka na kuwafuata wabunge kwenye viti vyao,
kiasi cha kufanya kuwepo na kile Spika alichokita kama ni vurugu ndani
ya Bunge.
Spika Anne Makinda alilalamika mara kadhaa kuwa
wabunge walikuwa wakifanya vurugu ndani ya ukumbi na kuwataka watulie,
kwani wengi walikuwa wanapishana kwenye viti vya wagombea akiwamo Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ambaye kiti chake
kilipata wageni wengi pia.
“Waheshimiwa wabunge naombeni utulivu basi, mbona
mnaleta vurugu kwa kutembea tembea humu ndani wakati kanuni hazisemi
hivyo, nitawataja kwa majina sasa,” alisema Makinda.
Karibu wagombea wote ambao ni wabunge, naibu
mawaziri na mawaziri jana walikuwa bungeni isipokuwa wagombea watatu wa
CCM ambao ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Nzega, Dk
Hamis Kigwangala na Mbunge wa Kisesa, Luhwaga Mpina ndiyo hawakuonekana.
Mapema mgombea urais, Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuvunja mwiko baada ya kuhama
katika kiti chake anachotumia kila siku na kumfuata mgombea mwenzake
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na wawili hao
walitumia muda mrefu wakizungumza pamoja.
Kutoka hapo, Mwigulu alianza kuzunguka kwa staili
yake kwa kwenda kwa wabunge huku akiwa makini kwa kukwepa viti
walivyokaa wagombea wenzake, ambao wakati wote nao walikuwa na wabunge
karibu yao wakizungumza.
Wagombea wengine waliokaa pamoja kwa muda mrefu
ndani ya ukumbi ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda baada ya Magufuli kumfuata Pinda katika kiti chake.
Mgombea mwingine ambaye jana alionekana kutotulia
katika kiti chake alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Kazi
Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.
Profesa Mwandosya huwa hana tabia ya kuhama kiti
chake na kuwafuata wabunge au mawaziri na badala yake hufuatwa alipo,
lakini jana hali ilikuwa tofauti.
Profesa Mwandosya alisalimiana na watu wengi ndani
na nje ya ukumbi wa Bunge, ambako alikutana na wabunge kadhaa wa Mkoa
wa Mbeya akiwemo mgombea mwenzake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe na waliteta kwa muda.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa wabunge wengi kufika kumsalimia anapokaa na haikuwa jambo geni
jana, kwani ni kawaida yake awapo ukumbini mara nyingi hukosa nafasi ya
kupumua kutokana na msururu wa wabunge.
|
June 24, 2015
WAGOMBEA URAIS WAHAMISHIA KAMPENI BUNGENI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment