![]() |
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa
lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana
akili na mpuuzi.
Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya
awali mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi
hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya
Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers,
vilivyopo Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi
kwamba ‘mimi Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule,
mjinga mmoja, amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana
akili yule’ alinukuu maneno hayo.
Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi
ya Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa
alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya
kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri
majina yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya
awali ya kesi inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya
mshtakiwa wa nne kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
Mbali na Gwajima wengine ni anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze na Georgey Milulu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa
Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar
es Salaam,washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya
Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa
mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu
cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura
ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Upande wa Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava
akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za
bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa
walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
CHANZO:
NIPASHE
|
July 21, 2015
GWAJIMA ASOMEWA MASHITAKA YA KUMTUKANA ASKOFU PENGO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment