KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

July 21, 2015

MAWAZIRI MAJI YA SHINGO MAJIMBONI.

Mawaziri kadhaa wa Rais Jakaya Kikwete wamekutana na upinzani mkali majimboni kutokana na kujitokeza kwa wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo yao kuomba uteuzi wa kugombea ubunge kupitia chama hicho.
 
Aidha, baadhi ya wabunge wa CCM wamekutana na upinzani mkali pia baada ya makada wenzao wengi kujitokeza majimboni kuomba kuteuliwa.
 
WASIRA- BUNDA MJINI (8)
Katika jimbo lililomegwa upya la Bunda mjini, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amepata wapinzani kupitia CCM ili waweze kupimana bana ubavu kuwania fursa ya kuongoza kwa kipindi cha miaka 
 
mitano ijayo.
Waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, mfanyabiashara Robert Maboto, Magesa Julius Magesa, Simoni Odunga, Peles Magiri, Isack Maela na Exvery Rugina.
 
FENELA MUKANGARA
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, atachuana na makada sita katika jimbo jipya la Kibamba. Makada hao ni George Shayo, Mashaka Sabaya, Rashid Mrisho, Issa Jumanne, Felix Mdeka na Goodvido Shayo.
 
DK. MWAKYEMBE
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, atakabiliana na ushindani kutoka kwa makada tisa wa chama hicho.
 
Makada hao ni Gabriel Kipija, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, John Mwaipopo, Prof.Leonard Mwaikambo, Gwakisa Mwandembwa, Vincent Mwamakingula, George Mwakalinga, Benjamin Richard, Asajile Mwambambale na Ackim Jackson.
 
DK. MARY NAGU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu, anayemaliza muda wake wa kiliongoza Jimbo la Hanang’ atakutana na upinzani kutoka kwa Peter Nyalandu, Aliamani Sideyeka  na Mayomba Dankani.
 
CHIZA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Cristopher Chiza, atakabiliana na makada sita waliojitokeza katika jimbo lake la Buyungu. 
 
ANNE KILANGO
Mbunge wa Same Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango, anakabiliwa na kibarua kugumu baada ya makada nane kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge.
 
Hao ni Michael Kadeghe, Dk. Eliji Kibacha, Semi Kiondo, Abraham Shakuri, Nyangasu Werema, Daudi Mambo na Ombeni Mfariji.
 
PROF. MAGHEMBE
Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Prof. Jumanne Maghembe, waliojitokeza kumpinga ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), Anania Thadayo, Karia Magaro, Baraka Lolila, Amani Kidali, Ramadhan Mahuna na Japhari Mghamba.
 
DK. KAMANI 
Mbunge aliyeangushwa na ndugu yake katika kura za maoni 2010, Dk. Raphael Chegeni ni miongoni mwa watia nia saba waliojitokeza kumrithi mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Titus Kamani.
 
Licha ya Dk. Chegeni na Dk. Kamani kuchukua na kurejesha fomu, pia wapo wanachama wengine wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Benard Kibese, Igo Shing’oma, Dasias Sweya, Robert Nyanda, Nyangi Msemakweli na Josephat Kwamba.
 
JUMA NKAMIA
Naibu wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makada 13.
 
Makada hao ni mwanahabari mwandamizi, Khamis Mkotya, Fredi Duma, Juliana Magembe, Juliana Maghembe, Juma Ilando, Yusuph Ibrahim, Idd Kisisa, Raphael Kelesa, Francis Julius, Godfrey Mayo, Pascal  Degera, Athman Hotty na Pascal Afa.
 
NYALANDU 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, anachuana na wagombea saba akiwamo Justine Monko, Michael Mpombo, Othman Mungwe, Amos Makiya, Yohana Eliyasini Too, Aron Mbogo na Sabasaba Manase.
 
MAJIMBO YA KIFO
 
BUKOBA MJINI
Jimbo la Bukoba Mjini lina ushindani mkali kutokana na makada nane kujitokeza wakiwamo Mbunge aliyemaliza muda wake, Balozi Khamis Kagasheki na hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Dk. Anatory Amani. 
 
Wengine ni Josephat Kaijage, George Rugahyuka, Filbert Katabazi, Elieth Projestus, Christina Rwezaura na aliyewahi kuwa Mbunge wa  jimbo hilo, Mujuni Kataraiya.
 
MULEBA KUSINI
Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleio ya Makazi, Prof. Anne Tibaijuka, ambaye ni Mbunge anayemaliza muda wake, Prof. Anne Tibaijuka, anakabiliwa na upinzani mkali baada ya makada tisa kujitokeza kuwania nafasi yake.
 
Mbali na Prof. Tinaijuka, wengine waliochukua na kurejesha fomu ni Dk. Adam Nyaruhuma, Stephen Tumain, Flavius Kahyoza, Buruan Rutabanzibwa, Muhaji Bushako, Kaino Mendes, Mnawaru Amoud na Erick.
 
IRINGA MJINI
Makada 13 wamejitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.
 
Wamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mahamudu Madenge.
 
Pia wamo Dk. Yahaya Msigwa, Nuru Hepautwa, Addo November Mwasongwe,  Adestino Mwilinge, Frank Kibiki, Aidani Kiponda,
 
Peter Mwanilwa, Fales Kibasa, Michael Mlowe na aliyetia nia ya kuwania urais, , Balozi Mstaafu Dk. Augustine Mahiga.
 
SHINYANGA MJINI
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Stephen Masele, amekutana na upinzani mkali, baada ya makada sita wa CCM kujitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.  
 
Wanaochuana na Masele ni Willy Mzanvas ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga na Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.
 
Wengine ni Dk. Charles Mlingwa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha; Hatibu Kazungu,Talla Mzeimana ,Abdallah Seni na Mussa Ngagara.
 

SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment