KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 4, 2015

MAGUFULI: POLISI ATAKAEUA JAMBAZI HATASHTAKIWA



Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema serikali yake haitamshtaki askari polisi ikiwa ataua jambazi mwenye silaha.
 
Mgombea huyo alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye  uwanja wa Mashujaa, mjini Mtwara.
 
Katika serikali yangu askari akimpiga jambazi mwenye silaha kwa risasi hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia vituo vya polisi, mbona hawavamii kambi za jeshi, Jeshi la Kujenga Taifa au Ukonga FFU?, wanaona polisi wana nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua,” alisema Magufuli.

Mgombea huyo wa urais wa CCM pia aliahidi kwamba ataboresha maslahi ya askari polisi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na wakiwa na furaha.

Kadhalika, aliahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais, atahakikisha makusanyo ya kodi kwa mwezi yanaongezeka mara mbili kutoka yanayokusanywa sasa ya Sh. bilioni 900 hadi Sh. tirioni 1.8.

Serikali ya awamu ya nne ilikuwa inakusanya mapato ya kila mwezi Sh. bilioni 300, lakini sasa yameongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 900 kwa serikali ya Magufuli nitahakikisha mapato yanafikia mara mbili ya haya,” alisema Dk. Magufuli.

Katika hotuba yake iliyoanza saa 10:12 jioni, mgombea huyo aliyekuwa akishangiliwa na umati uliojitokeza kumsikiliza sera zake, aliahidi pia kuwapatia wananchi maendeleo.

Alisema wingi wa watu waliojitokeza kumsikiliza unadhihirisha kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli ambayo yataletwa na CCM.

Kwa idadi hii kubwa ya watu inadhihirisha kuwa wana Mtwara na  Watanzania kwa ujumla sasa wanataka mabadiliko na siyo kusema mabadiliko tu bali ya kweli na ndiyo maana urais. 

Nilipoomba urais sikuwa najaribu, nimekuwa mbunge kwa miaka 20 hivyo naifahamu vizuri serikali  na nafahamu mahali serikali ilipolegea, nichagueni mimi niwatumikie,” alisema Dk. Magufuli.

Aidha, aliahidi  kujenga barabara zilizosalia kutoka Mtwara- Newala -Tandahimba hadi Masasi. Mbali na hilo, aliwaahidi wananchi wa Mtwara kuwa watajengewa bandari kubwa kama za Dar es Salaam na Tanga pamoja na viwanda.

Serikali ya Magufuli ni ya viwanda, serikali ya Rais Kikwete imejenga kiwanda cha saruji kinachomilikiwa na Dangote, mkinichagua nitamwaga viwanda vingi zaidi ili vizalishe na kutoa ajira kwa watu wengi,” alisema na kushangiliwa.

Awali jana akizungumza katika mkutano wa kampeni wilayani Tandahimba, mkoani Ruvuma kabla ya kwenda Mtwara, Dk. Magufuli, alisema anatambua shida wanaozopata wakulima wa korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuahidi kuzipatia ufumbuzi.

Wakulima wa zao hilo mikoa ya Kusini mwa Tanzania wamekuwa wakiulalamikia utaratibu huo kwa muda mrefu, wakisema ni wa kinyonyaji.

Dk. Magufuli pia aliahidi kutatua matatizo ya  wakulima wa korosho kucheleweshewa fedha, kulipwa nusu na uhaba wa dawa na pembejeo kuchelewa.

Akizungumza katika mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tandahimba, Dk. Magufuli alisema pia kuna wabadhilifu wa fedha za wakulima ndani ya vyama vya ushirika na kwamba serikali yake itaondoa kero hizo ili wakulima wanufaike na kilimo hicho.

Nimesomea Shahada ya Uzamivu ya masuala ya korosho, hayo ndiyo masuala yangu, mnatakiwa kunufaika na korosho na pia maganda yake yanaweza kutengeneza gundi na vitu vya kuzuia kutu, tutaongeza viwanda vikubwa vya korosho ili kuongeza thamani ya mazao yenu mnufaike,” alisema.

Alisema atahakikisha bei ya korosho inaongezeka kutoka ya sasa ya Sh. 300 kwa kilo moja.

Hapa Tandahimba kuna vyama vingi vya ushirika lakini havifanyi vizuri, tutaviimarisha vihudumie wakulima ipasavyo walipwe fedha bila kukopwa, wanaodokoa fedha nitawadhibiti,” alisema.

Akizungumzia gesi, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi kama gesi, mafuta, wanyama, madini na nyingine nyingi.

Alisema uchumi wa gesi utawezesha viwanda vingi kujengwa na watu kupata ajira.

Dk. Magufuli alisema gesi ni lazima inufaishe wananchi wa eneo husika kabla ya kunufaisha wengine.

Gesi imetoka hapa lazima wakazi wa hapa mnufaike kwanza, huwezi kuwa na gesi inufaishe wengine, mpate umeme wa uhakika, ajira na uchumi wetu ubadilike,” alisema.

Aidha, aliwatahadharisha wananchi hao dhidi ya nchi za Ulaya zinazonyemelea utajiri wa Tanzania na kwamba wasiruhusiwe kuwagawa Watanzania.

Siku zote vita ya panzi ni furaha ya  kunguru, mtu akihubiri ugomvi, chuki na kutokuwa na amani siyo mwenzetu, msikubali kuchonganishwa na wanaotumika na wanaozitamani rasilimali zetu,” alisema.

Alisema kugunduliwa kwa  gesi kutawezesha ujenzi wa viwanda vidogo,  vya kati na vikubwa kwa kuwa rasilimali hiyo inaweza kufanya mambo mengi ikiwamo Tanzania kuwa na kiwanda cha ndege.

Alisema kwa sasa kiwanda cha saruji cha Dangote kinaendelea kujengwa na kwamba pamoja na vingine kitasaidia bei ya vifaa vya ujenzi kupungua bei na kurahisisha wananchi kujenga nyumba nzuri na kisasa na vijana kupata ajira.

No comments:

Post a Comment