![]() |
Meneja Msaidizi wa Kituo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation Centre,Sophia Moshi akibadilishana mawazo na meneja mkuu wa kituo hicho,Claus Heim. |
……………………………………
Mahmoud Ahmad,Arusha
Serikali imeombwa kuchukua hatua
kali kwa baadhi ya wazazi nchini wenye tabia ya kuwaficha watoto wao
wenye ulemavu hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakose mahitaji ya msingi
kama elimu na afya.
Ombi hilo limetolewa hivi
karibuni na uongozi wa chuo cha walemavu cha Usa River Rehabilitation
Centre huku wakiiomba serikali iviangalie vituo vya kulea watoto
walemavu kwa kuvipatia ruzuku .
Akizungumza katika mahojiano
maalumu na gazeti hili chuoni hapo,meneja wa chuo hicho,Claus Heim
alisema kwamba serikali inapaswa kuhakikisha inawachukulia hatua kali za
kisheria baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wao wenye
ulemevu majumbani.
Alisema kwamba serikali inapaswa
kuweka sheria kali na kuhakikisha zinatekelezwa ili kuwapa fursa watoto
wenye ulemavu nchini kupata huduma za msingi kama elimu,afya,chakula
pamoja malazi.
“Hawa wazazi wanaowaficha watoto
wenye ulemavu nchini je wanachukuliwa hatua gani?kila mtoto ana haki ya
elimu na afya lakini nani anawajibika”alihoji Heim ambaye ni raia wa
nchini ujerumani
Hatahivyo,meneja msaidizi wa
kituo hicho,Sophia Moshi kwa upande wake alisema kwamba ni wajibu wa
serikali kuhakikisha inavipatia ruzuku vyuo vya ulemavu nchini ili
viweze kujiendesha kwa kuwa vinakabiliwa na changamoto lukuki.
Alisema kwamba mtoto mwenye
ulemavu ana uwezo kama mtoto mwingine na hivyo kuitaka jamii kuwathamini
watoto wenye mahitaji maalumu badala ya kuwanyanyapaa.
Mbali na kauli hiyo Moshi
alisema kwamba chuo chao kimejipanga kujenga shule ya sekondari kwa
lengo la kuongeza mapato ya kuendesha chuo hicho badala ya kutegemea
wafadhili ,kusajili kituo cha afya kwa ajili ya matibabu ya mguu
kifundo(club foot) sanjari na kusajili chuo cha ufundi chuoni hapo.
Chuo hicho kilianzishwa mnamo
mwaka 1988 na kinasimamiwa na kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT)
Dayosisi ya Meru ,kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 74 walemavu ambao ni
wasichana na wavulana ambapo nchi ya ujerumani ndiye mfadhili mkuu kwa
sasa.
No comments:
Post a Comment