![]() |
FREDY AZZAH, HANANG
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendele (Chadema), Edward
Lowassa, amesema akiingia madarakani, Serikali yake itawalipa posho
wenyeviti wa Serikali za vijiji, wenyeviti wa mitaa na wenyeviti wa
vitongoji kwa kuwa wanafanya kazi kubwa.
Lowassa ambaye jana alifanya mikutano mitano ya kampeni Magugu,
Dongobesh, Bashinet na Haidom, aliyasema hayo akiwa kwenye mkutano wa
kampeni Makondeko, Kateshi, wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.
“Serikali yangu ikiingia madarakani wenyeviti wa vijiji, vitongoji,
mitaa tutawalipa posho. Lazima tugawane keki ya nchi kwa sababu hawa
wanafanya kazi kubwa, lazima walipwe,” alisema Lowassa.
Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
alimpongeza mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kwa
kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nampongeza Kingunge kwa kukubali mabadiliko,” alisema Lowassa.
Akiwa kwenye mji mdogo wa Magugu, Lowassa alisema Serikali yake
itajenga hospitali mpya za kisasa zenye vifaa vyote na wataalamu.
Kuhusu elimu alisema wapo watu wanaokejeli sera ya kutoa elimu bure
kuanzia shule za watoto wadogo mpaka chuo kikuu wakihoji atapata wapi
fedha.
Kama nchi ina gesi, madini na inaweza kununua mashangingi haiwezi kushindwa kutoa elimu bure, alisema.
“Nagombea ili nipambane na umasikini, ninaamini hakuna urithi
utakaoweza kumpa mtoto wako kama siyo elimu ndiyo maana nasema
kipaumbele changu cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni
elimu,” alisema.
Baada ya elimu, alisema atahakikisha anaboresha kilimo ikiwa ni
pamoja na kutafuta soko la uhakika kwa bidhaa za wakulima na kuwaruhusu
kuuza mazao yao popote penye soko.
Naye Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, akiwa Magugu, alisema
kuna njama chafu zinaendeshwa za kuwaeleza wananchi siku ya kupiga kura
watakuta jina la Ukawa na siyo vyama vinavyounda umoja huo.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“Kwenye karatasi ya kura hamtakuta jina la Ukawa, mtakuta majina ya
vyama, rais mtampigia anatoka Chadema na wagombea wengine wako kwenye
vyama husika,” alisema Sumaye.
Aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanawahi kwenye vituo vya kupigia
kura ili wasikose fursa hiyo kutokana na njama za wapinzani wao wa
siasa.
Akiwa Kateshi, alisema baadhi ya viongozi wa CCM wanasema wanataka kufuta historia yake ya utendaji, jambo alilosema ni ndoto.
“Hawawezi hawa, mimi nilitoka madarakani nyama ilikuwa ikiuzwa kilo
moja Sh 500, sukari kilo Sh 600 na vitu vingine vingi bei ilikuwa chini.
“Kama wanataka kufuta historia yangu, wahakikishe wanashusha bei za
bidhaa viwe kama tulipokuwa sisi madarakani,” alisema Sumaye.
Alisema hata kwenye jimbo la Hanang, aliliacha likiwa na maendeleo
ikiwa ni pamoja na hospitali kuwa na dawa lakini kwa sasa hakuna tena
hizo huduma.
Akizunguzia hoja za Sumaye, Lowassa alisema wakati kiongozi huyo
akiwa CCM alidharauliwa lakini kwa sasa Tanzania nzima inamheshimu.
“Amejenga hoja nzuri ya CCM kutoendelea kubaki madarakani, CCM
walimdharau, lakini tangu aje Ukawa, Tanzania nzima inamtambua na
kumheshimu,” alisema Lowassa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Wilaya ya Hangang, Idi Kitiyanga, alirudisha kadi ya chama chake na kuchukua ya Chadema.
Kityanga aliyekuwa pia diwani wa Kata ya Masakta, alisema amechukua
uamuzi huo kwa kutambua kuwa hakuna mabadiliko yanayoweza kufanywa na
CCM.
No comments:
Post a Comment