………………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Smile Communications
Tanzania, imetangaza kupanua huduma ya mtandao wake wa intaneti ya 4G
LTE katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Moshi, Dodoma na Morogoro ikilenga
kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma ya internet yenye kasi katika
maeneo mengi zaidi nchini.
Upanuzi huo ulitangazwa rasmi
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hafla maalum
iliyohudhuriwa na waandishi wa habari, wateja wa kampuni hiyo pamoja na
wadau wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano hapa nchini wakiongozwa na
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dr. Ally
Simba.
Meneja Mkazi wa Smile
Communications Tanzania, Bw. Eric Behner alisema fedha za uwezeshaji wa
mradi huo ni sehemu ya Dola za Kimarekani milioni 365 ambazo kampuni
mama ya Smile Telecoms ilikusanya mwezi Septemba kwa njia ya ukopaji na
uuzaji wa hisa ili kufadhili upanuzi wa Intaneti yake ya kasi ya 4G LTE
katika nchi za Afrika.
“Hatua hii ni pamoja na upelekaji
wa huduma zetu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na zaidi
inatizamiwa kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, Smile Communications
tutakuwa katika nafasi ya kutoa huduma za sauti na huduma za uhakika
zitakazoweza kuwafikia watumiaji katika kila mkoa kati ya mikoa mitano
iliyoainishwa nchini,’’ alibainisha.
Uwekezaji huo unaelezwa kuwa ni
moja kati ya ukuzaji mtaji mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa na kampuni za
mawasiliano barani Afrika na inapelekea jumla ya uwekezaji ulioelekezwa
katika kutekeleza miradi ya Smile tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 na
kufikia takribani Dola za Kimarekani milioni 600.
Katika hatua nyingine kampuni
hiyo ilitangaza huduma ya kipekee maalum kwa ajili ya wateja wa
kibiashara iitwayo ‘Smile@business’ ambayo pamoja na mambo mengine,
itatoa fursa kwa makampuni kulipia kifurushi kimoja kitakachotumika na
watumiaji wengi bila kujali mahali walipo au kifaa wanachokitumia.
“Lengo letu kuu ni kuwa chaguo la
kwanza la watanzania katika huduma za intaneti ya kasi, na
kuwatengenezea wateja wetu nchini njia ya haraka, ya kuaminika na yenye
ubora wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta maendeleo
ya taifa kwa ujumla,’’ alisema Bw. Ahmed Seif , Mkuu wa kitengo cha
mauzo na masoko wa kampuni hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo,
Dr. Simba alisema upanuzi huo wa huduma za kampuni ya Smile
Communications Tanzania unakwenda sambamba na mpango wa serikali wa
kuhakikisha kwamba huduma ya mawasiliano ya internet yenye kasi zaidi
inafika kila kona ya nchi ndani ya kipindi kifupi kijacho.
“Lengo ni kuona kwamba unafika
wakati mtu aliyepo mkoa wa Katavi anakuwa kwenye mazingira ya kupata
huduma ya internet yenye ubora na kasi sawa na mtu aliyepo jijini Dar es
Salaam…ndio maana TCRA tunawapongeza sana watu wa Smile kwa hatua hii
waliyofikia,’’ alibainisha.
No comments:
Post a Comment