KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 12, 2016

WANAWAKE MWANZA WATAKIWA KUTOBWETEKA ILI KUACHANA NA UTEGEMEZI KATIKA JAMII.

Kulia ni Bi.Vileth Muhamusi ambae ni mmoja wa Wajasiriamali Jijini Mwanza akizungumza na Mwandishi wa taarifa hii, 
 …………………………………………………………………………….
Wanawake Mkoani Mwanza wametakiwa kutobweteka
na kukaa majumbani bila kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, kwa
kuwa hatua hiyo inawafanya kuwa tegemezi katika jamii.
 
Bi.Vileth Muhamusi ambae ni mmoja wa
Wajasiriamali maarufu Jijini Mwanza, anaejishughulisha na biashara ya bustani
hususani kuotesha miche mbalimbali ikiwemo miche ya mbao, matunda pamoja na
kimvuli, aliyasema hayo jana wakati akizungumzia tatizo la ukosefu wa ajira
kwa akina mama ambalo hivi sasa limegeuka janga kwa malezi ya watoto kutokana
na baadhi yao kuwatumia watoto wao katika shughuli za kuomba omba mitaani ili kupata
fedha za kujikimu kimaisha.
 
Bi.Muhamusi anaepatikana katika
bustani zilizopo pembezoni mwa Ziwa Victoria katika barabara ya Makongoro
Jijini Mwanza, alibainisha kwamba wanawake wanapaswa kuchukua hatua na kuachana
na fikra za utegemezi, ikiwemo kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo,
akitolea mfano kikundi chake kijulikanacho kama Mazingira Group, na kwamba kupitia
vikundi hivyo wanawake wataweza kupiga hatua za kimaendeleo.
 
Alianza shughuli zake za kuotesha
miche miaka mitano iliyopita, na ameweza kupata kipato cha kumuwezesha kujikimu
kimaisha yeye pamoja na familia yake huku kubwa zaidi likiwa ni kumudu kuwasomesha
watoto wake kutokana na biashara ya kuuza miche anayootesha, ambapo anabainisha
kwamba biashara hiyo inalipa kwani kuna aina mbalimbali za miche ambayo ina soko
kubwa, akitolea mfano miche ya Mitiki ambayo mche mmoja huuzwa hadi shilingi
elfu tatu.
 
Hata hivyo bi.Muhanusi aliwatoa hofu
wanawake juu ya suala la mitaji ambalo limekuwa likilalamikiwa na wengi, ambapo
ametanabaisha kwamba shughuli nyingi za ujasiriamali ikiwemo ya bustani, hazigharimu
mtaji mkubwa ikilinganisha na gharama za mahitaji yao ya kila siku kama vile
gharama za saluni huku wakiwa hawana shughuli za kuwaingizia kipato.
 
Kauli ya Bi.Muhanusi iliungwa mkono na
Edwin Soko ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Wajasiriamali Tanzania, aliebainisha
kwamba ili wanawake waondokane na utegemezi ni vyema wakajitambua na kufungua
fikra zao, kwani baadhi yao wamekuwa wakiwekeza katika matumizi mabaya ya fedha
ikiwemo kutumia hadi shilingi elfu sabini kwa ajili ya urembo huku wakiwa
hawana shughuli za uzalishaji mali, jambo ambalo linawakwamisha wengi wao kupiga
hatua za kimaendeleo. 
Mmoja wa Vijana wanaootesha mbegu
Miche ya aina mbalimbali
Picha na Hamza Makuza, BMG Mwanza.

No comments:

Post a Comment