Katika kuhakikisha
wanajitanua katika utoaji wa huduma bora za uhakiki na ukaguzi wa
hesabu, kampuni ya KLSA Associates ya nchini imejiunga na mtandao wa
kimataifa wa makampuni ya hesabu za kifedha na ushauri ya PKF ambapo
baada ya kujiunga imebadilika jina kutoka KLSA Associates na kuwa PKF
Associates Tanzania.
Akizungumza
katika halfa ya KLSA kujiunga PKF, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad aliwapongeza KLSA kujiunga na PKF
na kuwataka kuongeza juhudi na kuboresha huduma zaidi kwa kuzingatia kwa
sasa wamejiunga na kampuni ambayo inasifika duniani katika ukaguzi wa
hesabu, utunzaji wa hesabu za kifedha, ufumbuzi na ushauri wa masuala ya
kodi na kibiashara.
“Tunafahamu
jinsi PKF wanavyofanya kazi, mmepata nafasi ya kujiunga nao na
itarahisisha kwenu kupata hata taarifa nyingi hivyo ni wakati wa
kuonyesha kuwa ninyi ni bora katika kutoa huduma,” alisema Prof. Assad.
Nae
Meneja Mshirika wa PKF Associates Tanzania, Mustasir Gulamhussein
alisema wameamua kujiunga na PKF kwa kutambua uwezo wao wa kufanya kazi
katika maeneo mbalimbali duniani na wanaamini kujiunga kwao
kutawawezesha kujitanua katika utoaji wa huduma bora zaidi kutokana na
kuwa na wafanyakazi walio na uwezo.
“PKF
ni jina linaloheshimika na kutambulika katika uhifadhi wa taarifa za
kifedha ulimwenguni na kwa kuwepo Tanzania kunadhihirisha umuhimu wake
katika kuwahudumia wateja ambao wanapanua wigo wao kimataifa na
tunaamini tutakuwa zaidi katika kutoa huduma,” alisema Gulamhussein.
Kwa
upande wa Mkurugenzi wa PKF Kanda ya Afrika, Theo Veemark alisema KLSA
ni kampuni nzuri katika utendaji wao wa kazi za uhakiki na ukaguzi wa
hesabu hapa nchini na wanaamini kufanya kazi na KLSA kutawawezesha
kutanua huduma zao zaidi na kurahisisha utendaji wa kazi.
“Tunafuraha
kuwakaribisha KLSA katika familia ya PKF tunaamini kupitia muungano huu
tutaweza kutanua soko letu la kibiashara na kubadilishana mawazo ili
tuweze kuboresha huduma zetu zaidi,” alisema Veemark.


No comments:
Post a Comment