1.Makampuni
ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan
Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), tumesononeshwa sana na taarifa
iliyochapishwa na gazeti la kila wiki la MwanaHALISI katika toleo namba
332 la tarehe 28 Machi 2016 lenye kichwa cha habari, “Siri za Kikwete,
IPTL zafichuka ”; iliyoambatana na nukuu katika ukurasa wake wa mbele
inayosomeka “…hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga
alitembeza mlungula.”
2.Taarifa
hiyo iliyojaa uongo pamoja na kashfa nzito ya rushwa kwa IPTL/PAP na
kwa viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya nne na wengine ambao
bado wamo katika serikali hii ya awamu ya tano, imediriki kudai kwa
kunukuu maneno yafuatayo,….. “Sethi alitoa rushwa kila mahali, ikiwamo
Ikulu, ili kufanikisha mpango wake huo….Alihonga kila mtu. Alitoa rushwa
kwa kila aliyeona faili la Escrow. Hadi maofisa wa Ikulu na viongozi
waandamizi kutoka wizara ya fedha……..hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu
kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula. Ni BoT pekee, ambako
hakuhonga au kuombwa rushwa.”
3.Tungependa
kukanusha taarifa hizi za shutuma ya rushwa ambazo ni za uongo na
uzushi mtupu wenye lengo la kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo
Mwenyekiti Mtendaji, Bw. Harbinder Singh Sethi. Taarifa hizi zisizo na
chembe ya ukweli ndani yake zinalenga kuchafua sifa ya Ikulu ambayo ni
taasisi nyeti hapa nchini kwa kuihusisha na upokeaji rushwa ambayo ni
kosa la jinai kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu.
4.Isitoshe
taarifa hizi zimejaa habari za uongo zilizobuniwa kwa nia na madhumuni
maovu ya kuichafua sifa za kampuni za IPTL/PAP na mwenyekiti wake Bw.
Harbinder Singh Sethi pamoja na kuwachonganisha dhidi ya wananchi wa
Tanzania kwa kuwahadaa na kuwaaminisha Watanzania kuwa IPTL/PAP
inaendeshwa kwa misingi ya rushwa na udanganyifu, hivyo basi haistahili
kufanya biashara hapa nchini.
5.Awali
ya yote, tungependa kuutarifu umma wa Watanzania kwamba tuhuma za
rushwa ni tuhuma nzito na wala siyo za kunyamaziwa kabisa. Rushwa ni
moja kati ya makosa makubwa ya kijinai ambayo vyombo vya dola vinatilia
maanani sana. Hivyo basi, kampuni ya IPTL/PAP haiwezi kukaa kimya wakati
tuhuma kama hizi zikiendelea kuchapishwa dhidi yake, huku ikiwahusisha
viongozi waandamizi wa serikali, bila ya gazeti husika pamoja na
mwandishi wa taarifa hizo kutoa udhibitisho wowote wa tuhuma hizo.
6.IPTL/PAP
tunaamini kwamba taratibu zote za kukabidhiwa kampuni ya IPTL (ikiwemo
mali na madeni halali) zilifuatwa. Tunaamini katika utawala wa sheria
ambayo inazingatia haki za kila mtu. Hivyo basi, haitakuwa busara
kuendelea kunyamazia vitendo vya kiovu vya kuichafua kampuni yetu
vinavyofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kisingizio cha “uhuru
wa kutoa maoni” au “uhuru wa vyombo vya habari”. Kama vyombo vya habari
walivyo na uhuru wao, vivyo hivyo IPTL/PAP kama kampuni ina uhuru wa
kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi bila ya kubughudhiwa.
Kwa kutuhumu IPTL/PAP au viongozi wake kutoa rushwa, bila kuthibitisha,
ni kuihujumu kampuni ili isiweze kutekeleza majukumu yake ya kuchangia
ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu.
7.Mbali
na tuhuma za rushwa, takriban taarifa nzima ya gazeti hilo la
MwanaHALISI imejaa uongo uliokubuhu na uzushi usiokuwa na chembe ya
aibu. Sehemu ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI inadai na
kunukuliwa “Kampuni hiyo binafsi ilidai kuwa gharama za umeme zilikua
asilimia 22.3; na gharama za mtaji asilimia 30 zilikuwa dola za Marekani
38.16 milioni. Hata hivyo, Mahakama ilithibitisha kuwa gharama halisi
za mtaji wa IPTL zilikuwa chini ya dola za Marekani 1,000”. Tunapenda
kuwataarifu Watanzania kuwa hakuna mahakama yoyote duniani
iliyothibitisha madai haya na hii ndiyo sababu kuu ya mwandhishi wa
taarifa hii kashindwa kutaja ni mahakama ipi hiyo iliyothibitisha hayo
yanayodaiwa na kunukuliwa.
8.Sehemu
ya taarifa ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa
“Lakini fedha hizo zilichotwa kabla mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi na
katika mazingira ya udaganyifu; na kwa kutumia baadhi ya nyaraka ambazo
ziligundulika kuwa ni za kugushi… Hata hivyo Sethi alishindwa kuweka
uthibitisho wowote kuwa kampuni hiyo inamiliki hisa za kampuni ya
Mechmar Limited ya Malaysia ndani ya IPTL.”
Kwa
yeyote aliyesoma Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) iliyojulikana
kama “Taarifa ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika
katika Akaunti ya “Escrow” ya Tegeta, Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya
IPTL”, anaweza kutambua kuwa tuhuma na madai yaliyonukuliwa hapo juu ni
uongo mtupu. Ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ukurasa wake
23 inaeleza kuwa Bw. Harbinder Singh Sethi aliwasilisha “Deed of
Assignment of Shares” na Mkataba wa Kuuza na Kununua hisa kati ya PAP na
PiperLink Investment kutokana na agizo la kuwasilisha ushahidi wa
kununua asilimia 70 za hisa za Mechmar katika IPTL. Si Mkaguzi Mkuu wa
Serikali wala chombo chochote cha serikali kilichopata kuthibitisha kuwa
nyaraka zilizowasilishwa na Bw. Harbinder Singh Sethi zilikuwa ni za
kughushi kama taarifa ya gazeti la MwanaHALISI ilnavyodai na kunukuliwa
hapo juu.
9.Sehemu
ya taarifa ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa
“Malipo hayo kwa PAP yalifanyika bila Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter
Muhongo, wala BoT kuhakiki uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP;
bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili
Kituo ch Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi
(TIN).” Hizi nazo ni taarifa za uongo zisizokuwa na chembe ya ukweli.
Mwandishi amejaribu kutumia mseto wa hoja zisizokuwa na mshiko ili mradi
anajenga taswira kuonyesha malipo yaliyofanywa kwa PAP yalikuwa ni
malipo ya ubabaishaji.
10.Sehemu
ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa
“Serikali ililazimika kukopa “kwa siri” kiasi hicho cha fedha kutoka
Stanbic kwa kuweka dhamana ya hati fungani, ili kufanikisha
upatikanajiwa fedha za kumlipa Singasinga wa IPTL,” ameeleza mmoja wa
maofisa wa Stanbic ambaye ametoka katika benki hiyo hivi karibuni. […]
Kigogo huyo anasema, “kwa vile wakubwa walishapanga kumlipa Sethi, kabla
ya Desemba 2013, ikabidi wakope benki kwa kuweka dhamana hati fungani
zilizoshushwa bei (discounted treasury bills).”
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (iliyotajwa hapo juu)
kwenye ukurasa wake wa 16 inaelezea wazi kabisa kuwa umiliki wa hati
fungani zilizowekezwa na BoT kutokana na fedha zilizokuwa kwenye akaunti
ya Escrow ya Tegeta, ulihamishwa kwenda kwa PAP tarehe 6 Desemba, 2013.
Madai ya kuwa serikali ilikopa kwa kuweka hati fungani zilizoshushwa
bei ni uongo na uzushi usiokuwa na ukweli wowote.
11.Sehemu
ya taarifa hiyo ya gazeti la MwanaHALISI imeendelea kudai na kunukuliwa
“Taarifa zinasema, katika kiasi hicho cha dola 180 milioni, dola
takriban 100 milioni, kilitoroshewa nje katika nchi za Falme za Kiarabu,
huko Dubai na Afrika Kusini, kabla ya kuhamishiwa tena nchini Austria.
Nchini Austria, taarifa zinasema, ndiko ambako mtoto wa mmoja wa
waliokuwa viongozi wa juu serikalini, amefungua akaunti.” Hizi ni
taarifa za uongo zisizokuwa na chembe ya ukweli na ni tuhuma zisizokuwa
na ushahidi wowote.
12.Kwa
machache haya ya uongo na uzushi tuliyoyanukuu na mengine mengi ambayo
tumeamua kutokuyatolea ufafanuzi kwa nia ya kuiweka taarifa hii kwa
ufupi, tungependa kuomba vyombo husika kuchukua hatua dhidi ya
waliohusika na uenezi wa taarifa hizi za kizushi kwa kuwafikisha mbele
ya vyombo vya dola na kuwahoji ili ukweli wa tuhuma ujulikane. Tunaamini
kwamba tabia ya kuikashifu kampuni yetu na kuwakashifu viongozi wa
serikali bila ya kuwa na uthibitisho isipokomeshwa, basi nchi itajaa
waropokaji na heshima ya serikali na vyombo vyake itaporomoka. Tabia hii
isipokomeshwa itaathiri hali ya uwekezaji nchini kwani itawakatisha
tamaa wawekezaji wengine wanaotaka kuwekeza nchini.
13.Kwa
muhtasari, taarifa zilichochapishwa kwenye makala husika ni uzushi
usiokuwa na ukweli wowote. Tungewaomba Watanzania na wote waliosoma au
watakaosoma makala husika wazipuuzie taarifa hizo. Pia tunawataka
wahariri na wachapishaji wa gazeti la MwanaHALISI kuomba radhi kwa
taarifa hizo za kizushi ndani ya siku kumi na nne (14). Kushindwa
kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kulifikisha
gazeti, wahariri na wachapishaji wake mahakamani.
14.IPTL/PAP
tuko tayari kutoa ushirikiano kwa mtu yeyote mwenye ushahidi wa rushwa
kufikisha mbele ya vyombo husika na kuhakikisha rushwa inakomeshwa.
15.Tunaomba
pia vyombo mbalimbali vinavyohusika na kulinda amani na utengamano wa
nchi yetu ikiwemo jeshi la polisi kuwachukulia hatua mwandishi wa makala
hiyo na wahariri wa gazeti la MwanaHALISI kwa kuvunja sheria za nchi
kwa kuandika habari za uchochezi.
Ahsanteni sana.
Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited
No comments:
Post a Comment