Tunayo furaha kubwa kuwakaribisha
kwenye Kongamano la Uwekezaji kati ya Watanzania na Warusi
litakalofanyika siku ya Ijumaa tarehe 28 Aprili 2016 katika Ukumbi wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Kongamano hili limeandaliwa na
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikishirikiana na Russian Export
Club, Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ubalozi wa Tanzania nchini
Urusi na Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania; kwa usimamizi wa Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji nchini Tanzania, Wizara ya Biashara na
Viwanda ya Urusi na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kongamano la Uwekezaji kati ya
Tanzania na Urusi 2016 linatarajia kuwaleta pamoja kundi la wawakilishi
wa Serikali ya Urusi, wenye viwanda na wafanyabiashara wakubwa kwa lengo
kushirikiana na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya
nchi hizi mbili. Kupitia mahusiano haya ya ushirikiano wa kiuchumi baina
ya Tanzania na Urusi kutaongeza zaidi ushiriki wa makampuni ya Kirusi
katika kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Ujumbe wa wafanyabiashara wa
Kirusi unatarajiwa kufikia watu 60 ukiongozwa na Mheshimiwa Denis
Manturov, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Serikali ya Shirikisho ya
Urusi. Ujumbe huu pia utajumuisha viongozi wengine wa serikali, Wakuu wa
makampuni na wawakilishi wa vyombo vya habari kutoka Urusi. Kongamano
hili litajikita zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi katika sekta za
nishati, usafirishaji, miundombinu, mafuta & gesi, madini, huduma za
fedha, kilimo na viwanda.
Wakati wa Kongamano hili,
yatafanyika majadiliano ya moja kwa moja na mikutano ya
Biashara-kwa-Bisahara (B2B), mikutano ya Serikali na Wafanyabiashara
(B2G) na Serikali na Serikali (G2G). Wafanyabiashara wa kutoka Urusi
watapata pia fursa ya kutembelea maeneo ya viwanda ya EPZA ili kujionea
uzoefu wa moja kwa moja kuhusu sekta ya viwanda hapa nchini.
Ushirikiano baina ya Tanzania na
Urusi katika nyanja za Uwekezaji na Biashara unaonesha kuwa mzuri kwa
miaka ya hivi karibuni ingawa bado ni mdogo ukilinganisha na fursa
zilizopo. Hivyo basi, kwa kupitia Kongamano hili, tutatoa nafasi ya
kufungua na kujionea fursa lukuki zilizopo za kiuwekezaji na kibiashara
baina ya nchi hizi mbili, pamoja na kukuza utalii.
Tunawakaribisha sana Wafanyabisahara wa Tanzania!
Imetolewa na: Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Tarehe: 26 Aprili 2016
No comments:
Post a Comment