![]() |
| JAJI MKUU wa Tanzania, Mohammed
Chande Othman amesema sheria ya mitandao ilipitishwa kwa lengo jema la
kulinda watumiaji, wanajamii na usalama wa Taifa la Tanzania.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi,
Mei 14, 2016) wakati akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa Watanzania
waishio Uingereza kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania
jijini London, Uingereza.
Alisema watu watatu kati ya wanne
nchini Tanzania wakiwemo watoto, wanamiliki simu za mkononi ambayo ni
sawa na watu milioni 35 kati ya milioni 45.
Alisema sheria hiyo ilitugwa kwa
misingi mitatu moja ikiwa ni kumpa mtumiaji uhuru wa kutoa maoni au
taarifa, uhuru ambao alisema unalindwa kikatiba lakini akaonya kuwa kila
uhuru unaotolewa pia una mipaka yake kama ilivyoainishwa kwenye ibara
ya 30(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema sheria hiyo pia inatoa
uhuru wa mtu kuwa na faragha (privacy) na msingi wa tatu ni sheria hiyo
kuzingatia matumizi ya mitandao ili kulinda usalama wa nchi.
“Sheria hii inakupa uhuru wa
kutumia mtandao kumlinda mwanajamii wenzako. Hapa Uingereza nimeongea na
mwendesha mashtaka mkuu ambaye aliniambia kuwa asilimia 60 ya makosa
yanayofanyika chini ya sheria ya makosa ya kujamiiana (Sexual Offencea
Act) yanatokana na mitandao,” alisema Jaji Mkuu wakati akijibu swali
kuhusu sheria ya makosa ya mitandao.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk.
Augustine Mahiga alisema kuitishwa kwa mkutano wa kupambana na rushwa
nchini Uingereza ni mojawapo ya jitihada za Waziri Mkuu wa nchi hiyo
kuanzisha vuguvugu la uanaharakati wa mapambano dhidi ya rushwa.
“Kukosekana kwa utawala bora,
changamoto za ugaidi, biashara za dawa za kulevya, biashara ya
kusafirisha binadamu na uwepo wa rushwa na ufisadi ni baadhi ya mambo
yaliyofanya dunia ibadilike. Haya mambo zamani yalikuwa hayana mahali pa
kuzungumzwa, kwa hiyo vikao kama hivi vitasaidia kukabili tatizo hili,”
alisema.
“Rushwa ni kama pweza mwenye vichwa vingi na mikia mingi. Waziri Mkuu David Cameron ameamua kuanzisha movement hii ili kutafuta njia za kukabili janga hili kubwa,” alisema.
Sote tunatanbua kuwa mataifa
mengi yangependa kuwemo katika hii movement lakini ni faraja kuona
kwamba Tanzania imo miongoni mwa waanzilishi na hii ni kwa sababu ya
uongozi nz ujasiri wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye kwa kweli ni game changer
(akimaanisha kuwa amebadili mwelekeo wa Taifa hili) kwani ana utashi
wa kisiasa na ana ujasiri wa kukemea maovu,” alisema huku akishagiliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu
wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola alisema vita ya rushwa nchini
Tanzania ni endelevu na inafanyika kuitikia wito alioutoa Rais Magufuli
wakati akizindua Bunge la Tanzania Novemba 20, 2015.
Alisema wanatumia mbinu
mbalimbali kupambana na rushwa lakini kubwa wanayoenda nayo hivi sasa ni
kutoa elimu kwa watoto na vijana ili kuwabadilisha tabia na utamaduni
uliojikita kwenye jamii.
|
May 16, 2016
JAJI MKUU: SHERIA YA MITANDAO INA LENGO ZURI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment