![]() |
Hussein Makame-MAELEZO
UIMARISHWAJI
wa miundombinu na uboreshaji wa sekta ya usafiri ni baadhi ya mihimili
inayopewa umuhimu nchini katika kuleta maendeleo ya wananchi na taifa
kwa ujumla hasa pale usafirishaji unapowezesha abiria na mizigo kufika
sehemu kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Juhudi
za Serikali ikiwemo Serikali kuu, Serikali za mitaa, taasisi za ndani
na nje ya nchi, mjenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa
pamoja zimekuwa zikishirikiana kuimarisha mtandao wa barabara ya kutosha
kwa nia ya kuwafikia wananchi wote na katika viwango bora.
Wachumi,
wanaeleza kuwa ili taifa lolote liweze kujikwamua kiuchumi ni lazima
pamoja na mambo mengine liboreshe sekta ya usafiri kuanzia ndani na nje
ya miji ili kurahisisha usafirishaji na kuchangia maendeleo.
Tanzania
inatajwa kuwa ni nchi inayoongoza kwa msongamano mkubwa wa magari
katika nchi za Jangwa la Sahara huku jiji la Dar es Salaam likiongoza
kwa msongamano mkubwa kutokana na kasi ya kuongezeka kwa wahamiaji
mijini huku miundombinu yake ya barabara ikibakia ile ile.
Hali
hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja
na taifa kwa ujumla mbali na athari za kiafya na kijamii zinazochangiwa
na moshi wa magari na kukaa sana kwenye gari wakati wa asubuhi na
jioni, hasa kwa wale wanaokaa mbali na sehemu zao za kazi.
Kukamilika
kwa barabara katika mfumo wa kisasa wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo
Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam kumewezesha kupatikana kwa
kilomita 20.9 za barabara.
Kilomita
hizo ni za barabara kutoka Kimara hadi Kivukoni Ferry, Morocco hadi
Magomeni na Fire hadi Kariakoo na miundombinu yake ikiwemo karakana na
vituo vikuu vya mabasi hayo.
Ujenzi
huu wa barabara ni kielelezo chanya kuelekea mafanikio ya kuleta
mabadiliko ya miundombinu ya usafiri jijini Dar es salaam katika muda
mfupi ujao.
BRT
ni mfumo unaoinukia kwa kasi duniani kwa kusafirisha haraka abiria wengi
mijini kwa gharama ndogo kwa kulinganisha na ule wa garimosho za mjini.
Utafiti
uliofanywa na Wakala wa Mradi wa Usafiri wa Haraka (DART) hivi karibuni
unaonesha kuwa foleni za magari barabarani hupoteza Shilingi Bilioni
655 kwa mwaka nchini na kusababisha changamoto nyingi.
Changamoto
hizo ni kupata magonjwa ya akili na maradhi ya mfumo wa hewa
inayochangiwa na kukaa sana kwenye magari na kuvuta moshi wa magari kwa
muda mrefu njiani kutokana na foleni.
Tafiti
mbalimbali zilizofanywa kuhusu usafiri wa jiji hilo zimebainisha maeneo
56 yanayokabiliwa na changamoto za usafiri ikiwemo kuwepo kwa mfumo wa
barabara ambao haukidhi mahitaji na hivyo kukosa uwezo wa kuhimili
usafiri wa umma.
Mbali
na msongamano wa magari, pia inaelezwa kuwa jiji hilo linakabiliwa na
kuwepo kwa vyombo vya usafiri vibovu, visivyokidhi mahitaji ya jamii ya
wakazi, na upande mwingine taa za kuongozea magari ambazo mara kwa mara
zinakuwa mbovu na zilizopitwa na wakati.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Mradi wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo
Haraka (BRT) ya mwaka 2003, msongamano wa magari husababishwa na wingi
wa daladala, ongezeko kubwa la magari ya watu binafsi, uendeshaji
usiozingatia kanuni na utendaji mbovu kwa baadhi ya askari waongoza
magari.
Ripoti
hiyo pia inaonesha kuwa jiji la Dar es Salaam lilikuwa na kilomita 450
tu za lami ambazo ni asilimia 39.5 ya kilomita 1,140 za barabara, wakati
kilomita 265 tu ndizo zilizokuwa zinatumika katika usafiri wa mabasi
jijini humo.
Kwa
upande wa vyombo vya usafiri wa umma, ripoti hiyo inaonesha kuwa
asilimia 90 ya magari hayo yana umri unaozidi miaka 10 na mengi ni
chakavu na hutumia muda mwingi barabarani na kwenye karakana kwa ajili
ya matengenezo.
Ripoti
hiyo inabainisha changamoto nyingine kuwa,ni ongezeko la kasi la
magari, zikiwemo daladala kwa zaidi ya miaka 16 iliyopita huku kukiwa na
usimamizi duni wa magari usiokuwa na mabadiliko wala mkakati mpya mbali
na kuwepo na mabadiliko hayo katika jiji.
Baada
ya kubaini changamoto hizo, wataalamu wa kizalendo wa jiji la Dar es
Salaam walianza kuweka mikakati ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo
na hivyo kuiunda DART chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI wakati
huo.
Lengo
la kuanzishwa kwa wakala hiyo lilikuwa ni kutaka kutoa huduma bora ya
usafiri kwa gharama nafuu katika jiji la Dar es salaam, ambalo ni ni
kitovu kikuu cha biashara nchini.
Katika
kutekeleza azma hiyo DART ilipanga mkakati wa kuwa na miundombinu bora,
inayokubalika kimataifa, yenye manejimenti ya oporesheni ya
usafirishaji.
Suala
la miundombinu ya barabara ilikabidhiwa TANROADS na kuanzisha kitengo
cha BRT ili kujenga mfumo huo unaoelezwa kuwa bora kiufanisi zaidi
duniani ulioanzia katika miji ya Curitiba (Brazili), Quito (Equador) na
Bogota (Colombia), na baadaye kuingia nchi za ulaya kama Ufaransa.
KWA NINI USAFIRI WA MABASI YA HARAKA (BRT)
“BRT ni aina ya usafiri wa mijini ambao ni nafuu na endelevu kuliko aina nyingine yoyote ya usafiri katika ulimwengu wa leo”
Haya
ni maneno ya utangulizi kwenye kitabu cha Ripoti hiyo ya mwaka 2003
yaliyoandikwa na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas
Masaburi.
Mbali
na kuwa nafuu na endelevu, BRT inaelezwa kwamba ni mfumo wa usafiri
unaohudumia watu wengi kwa haraka na hutumia njia maalum na mabasi
makubwa yenye uwezo wa kusafirisha abiria wengi hadi 48,000 kwa saa kwa
mwendo wa zaidi ya kilomita 22 kwa saa.
Mfumo
wa BRT unazingatia mahitaji ya watumiaji wengine wa barabara waenda kwa
baiskeli, watembea kwa miguu na huduma maalum kwa walemavu na
miundombinu yake hutumika kupunguza muda wa safari.
Moja
ya malengo makuu ya mradi huo ni kubadilisha sura ya jiji kwa kuboresha
matumizi ya maeneo ya kandokando ya njia kuu ya mradi na kurahisisha
maendeleo ya kiuchumi kwa jiji zima.
Kuanzishwa kwa mradi wa BRT kumetokana na kukosekana kwa mradi wa mabasi madhubuti unaokidhi mahitaji yote ya usafiri.
HALI YA USAFIRI WA JIJI LA DAR ES SALAAM
Ongezeko
la watu katika jiji la Dar es Salaam linachangia changamoto za sekta ya
usafiri na takwimu zinaonesha kwa miaka 20 ijayo, jiji hilo
linatazamiwa kuwa na watu 7,614, 459 watakaohitaji huduma ya usafiri.
Inaelezwa
pia wakazi wengi wa jiji hilo hupendelea kutumia usafiri wa umma
kutokana na sababu za kiuchumi.Hivyo kuanzishwa kwa BRT kutasaidia
wananchi wengi wenye kipato duni.
Pia
imebainika kwamba abiria wengi na magari mengi yanatumia barabara kuu
huku msongamano mkubwa ukiwa katika barabara ya Morogoro ikifuatiwa na
Barabara ya Kawawa na Uhuru.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, Barabara ya Uhuru miaka 10 iliyopita ilikuwa na
abiria wengi kwa kuwa na abiria 15,000 na magari 770 kwa saa, ikifuatiwa
na barabara ya Morogoro yenye abiria 9,000 na magari 715.
Barabara
ya Kilwa ilikuwa na 6,200 kwa 549, Kawawa 10,000 kwa 383 kwa saa,
Barabara ya Nyerere 8,600 na magari 399 kwa saa na Barabara ya Ali
Hassan Mwinyi abiria5100 na maagari 281 kwa saa.
Inaonesha
pia abiria wengi wanaoelekea katikati ya jiji asilimia 43 hutumia
usafiri wa umma, na asilimia 6 hutumia magari binafsi.
Daladala
hubeba takrbani abiria mil 1.4 kwa siku huku abiria wengi wakielekea
Kariakoo, katikati ya mji (Posta) na hospitali ya Muhimbili na mengine
ni Ubungo, Mwenge na Kimara.
UTEKELEZAJI WA MAMBO YA MRADI WA BRT
Utekelezaji
wa mradi wa BRT utafanywa kwa awamu sita ambapo awamu ya kwanza
imeshakamilika na huduma imeanza kutolewa baada ya kufikia makubaliano
juu ya maslahi ya wananchi na Umma kwa ujumla.
Awamu
hii ya kwanza inaanzia na Barabara ya Morogoro na Kawawa, ikifuatiwa na
Barabara ya Uhuru na Nyerere, na Kilwa na ifikapo mwaka 2035
inategemewa asilimia 91 ya wakazi wa jiji wataweza kupata huduma ya
mradi huo.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Mradi wa BRT, awamu ya kwanza inahusisha
njia kuu na lishi zenye mtandao wa barabara wa kilomita 20.85, vituo vya
kawaida 29,vituo vikuu 5 na karakana 2 za Ubungo na Jangwani.
Mpango wa muda mrefu wa BRT ni kuwa na kilomita 137 za njia maalum ya mabasi na vituo 18 na vituo vya kawaida 228.
Tayari
vituo vikuu viwili vimejengwa vya Kivukoni karibu na kituo cha Kivuko
cha Kigamboni na Soko la Samaki na cha Ubungo karibu na Kituo Kikuu cha
Mabasi yaendayo Mikoani (UBT).
Vituo
vingine vilivyokwishajengwa ni Ubungo, Kimara (Kimara mwisho), Kariakoo
(mtaa wa Msimbazi na njia ya Reli) na Morocco ambapo kila kituo
kitahudumia mabasi 65 kwa saa kwa kila mwelekeo.
Mabasi
ya njia kuu yatakuwa aina ya kumbakumba yenye uwezo wa kubabe abiria
140 na kila basi litakuwa na safari ya kilomita 14 kila siku.
NJIA KUU ZA MRADI WA MABASI AWAMU YA KWANZA
Lengo
la BRT ni kusafirisha abiria wengi kwa muda mfupi, kufupisha muda wa
kusimama vituoni kwa kuimarisha usafiri wakati wa asubuhi na jioni
ambapo maahitaji ya awali yalionesha huduma ya mabasi 40 kwa saa na
katika vipindi vya kawaida mabasi 10 kwa saa (kila baada ya dakika 5)
Ilielezwa
kuwa usafiri wa BRT utakuwa na safari 7 kupitia njia saba katika
barabara kuu, safari za haraka 2 na safari 5 za kawaida na muda wa kazi
ni kuanzia saa 11 alfajiri mpaka saa 5 usiku kila siku.Hata hivyo
huwenda muda huo ukafanyiwa mabadiliko kulingana na mahitaji.
Kwa mujibu wa DART kila njia kuu itakuwa na vituo vya kusimama kwenye vituo maalum kama inavyoonesha hapo chini.
DR001-UBUKOO,
ni njia inayohusu mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha
Ubungo na Kituo Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 15
na kuhudumia abiria 3,329 asubuhi na jioni 1,880 kwa mzunguko wa dakika
47.
DR002-KIMKOO,
inahusu mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Kimara na Kituo
Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 14 vya Kimara
terminal, Resort, Thomas, Baruti, Corner, Kibo, Ubungo, Tanesco, Kituo
Kikuu cha Ubungo, Bakhressa, Baptist Church, Fire, Uhuru Street na Kituo
kikuu cha Kariakoo).
Abiria
wa asubuhi wanakadiriwa kufikia 6,801 na jioni abiria 3,505 na mabasi
hayo yatatumika kwa mzunguko wa dakika 67 na itatoa huduma ya haraka
yaani service index katika kiwango cha asilimia 43
Njia
ya DR003-KIMKIV, ni ya mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha
Kimara na Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote 26
ikiwemo vya Kimara terminal, Korogwe, Bucha, Resort, Thomas, Baruti,
Corner, Kibo, Ubungo Tanesco, Kituo Kikuu cha Ubungo, Shekilango,
Urafiki, Manzese Tipo Top, Bakhressa, Manzese Agentina, Kagera,
Mwembechai, Usalama, Baptist Church, Jngawani, Fire, DIT, Kisutu,
Nyerere Square, Posta ya Zamani, Kivukoni na Magogono Ferry.
Abiria wanaotegemewa kusafiri ni 7,215 wakati wa asubuhi na jioni ni abiria 3,048 na watatumia dakika 82 kwa mzunguko.
DR004-MORKOO,
ni njia inahusisha mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha
Morocco na Kituo Kikuu cha Kariakoo na yatasimama katika vituo vyote 12
(Morocco, Kinondoni B, Mwanamboka, Mkwajuni, Kanisani, Magomeni
Hospitali, Baptist Church, Jangwani, Fire, Uhuru Street na Kituo kikuu
cha Kariakoo) na mzunguko wa safari ni dakika 38.
DR005-MORUBU,
ni njia ya abiria wanaosafiri kati ya Kituo Kikuu cha Morocco na Kituo
Kikuu cha Ubungo ambapo mabasi yatasimama katika vituo vyote 16.Asubuhi
inategemea kusafirisha abiria 6,189, jioni abiria 3,419 na itatumia
mzunguko wa dakika 24.
DR006-MORKIV,
inahusisha mabasi yanayotoa huduma kati ya Kituo Kikuu cha Morocco na
Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote 25.Asubuhi
inategemea kusafirisha niabiria 2,935 na jioni abiria 1,928.Njia hii
itakuwa na mzunguko wa dakika 46.
DR007-,
UBUKIV.Hii ni njia ya mwisho itakayosarisha abiria kati ya Kituo Kikuu
cha Ubungo na Kituo Kikuu cha Kivukoni na yatasimama katika vituo vyote
12 vya Ubungo terminal, Shekilango,Urafiki, Mahakama, Bakhressa,
Magomeni Kagera, Fire, Bibititi, Libya, City Council, Posta ya Zamani,
na Kivukoni terminal).
Inategemea
kuwa na abiria 2,726 asubuhi na jioni abiria 1,766. Nji hii itachukua
mzunguko wa safari wa dakika 25 na inategemewa kutoa kiwango cha huduma
ya haraka kwa asilimia 38.
Vituo
hivi saba vitatoa huduma ya urefu wa kilomita 145.8.Hata hivyo ili
kuendana na viwango vinavyohitajika na huduma kuwa endelevu, basi moja
linatakiwa kusafirisha abiria 2,000 kwa siku.
Safari
zote zitachukua jumla ya mabasi makubwa 116 ikiwemo mabasi 6 ya akiba
na mabasi lishi 237 na inakadiriwa kuwa abiria 350,000 watasafirishwa
kila siku.
Kuhusu
nauli, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART),
David Mgwasa anasema nauli za mabasi zitakuwa shilingi 200 kwa
mwanafunzi, shilingi 650 kwa njia maalum na kwa njia lishi nauli ni
shilingi 400 na wanaounganisha njia zote za lishi na maalum watalipa
shilingi 800.
Abiria
watanunua tiketi zao kwa keshia nayepatikana kwenye kila kituo cha
mabasi hayo au watanunua kadi ambayo ataipangusa (tap) kwenye mashine
iliyopo kituoni na kupewa tiketi.
Anasema
UDART kwa sasa iko kwenye mchakato wa kuhakikisha abiria anaweza
kulipia nauli kwa kutumia simu ya mkononi au kupitia benki.
|
May 12, 2016
MAKALA YA MABASI YAENDAYO HARAKA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment