![]() |
| Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) Dkt. Jabiri Bakari akiwa katika moja ya majukumbu yake.
……………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
SERIKALI kupitia wakala ya
Serikali mtandao imesema kuwa inaendelea kulifanyia kazi suala la
uanzishaji wa mfumo wa TEHAMA utakaowawezesha wananchi kupata huduma na
taarifa mbalimbali za Serikali kupitia simu zao mkononi mahali popote
walipo kwa njia ya mtandao.
Utaratibu huo pia utawawezesha
wahitimu wa vyuo mbalimbali vya elimu nchini Tanzania kupata taarifa za
ajira za Serikali na kuwawezesha kuomba nafasi hizo, kufuatilia majibu
ya usaili walioufanya na kupata taarifa za kuitwa kazini kupitia namba
za utambulisho watakazopewa kupitia ujumbe mfupi (sms).
Akizungumza na Wahariri wa vyombo
vya Habari leo jijini Dar es salaam Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali
Mtandao (e-Government Agency) Dkt. Jabiri Bakari amesema kuwa mfumo
huo utamuwezesha mwananchi kupata huduma za Serikali mahali popote alipo
kufuatia mifumo ya TEHAMA kuwasiliana na kubadilishana taarifa.
Amesema kuwa dhana ya Serikali
Mtandao ni kuwa na matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli zote za Serikali
kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwenye
huduma za Afya, Utalii, Malipo ya tozo za huduma,vibali, leseni ,elimu
na huduma mbalimbali za Serikali.
Dkt. Jabiri amesema moja ya vitu
vinavyosababisha usumbufu kwa wananchi kutokana na kukosekana kwa
Serikali mtandao ni pale wanapohitaji kupata huduma za Serikali ikiwemo
Hati ya kusafiria ambapo hulazimika kwenda Idara ya Uhamiaji kujaza fomu
maalum na kisha kusubiri kwa muda wa zaidi ya wiki moja ili taarifa zao
ziweze kuhakikiwa na taasisi nyingine za Serikali wakati suala hilo
lingeweza kuchukua siku moja.
“Matumizi ya TEHAMA kwenye
shughuli za Serikali hurahisiaha sana upatikanaji wa taarifa kwa kuwa
mifumo inawasiliana na kubadilishana taarifa haimlazimu mwananchi kwenda
kwenye taasisi zaidi ya tano kupata huduma yake” Amesisitiza Dkt.
Jabiri.
Amesema taasisi za Serikali kama
Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya
Uhamiaji, RITA na taasisi nyingine ambazo majukumu yao hutegemeana
kupitia serikali mtandaomifumo ya taasisi hizo huunganishwa ili ifanye
kazi pamoja kwa lengo la kuruhusu mifumo kuzungumza kumuhudumia
mwanachi bila yeye kulazimia kuzifuata taasisi hizo.
Amesema kuwa pamoja na maboresho
mbalimbali yanayoendelea ndani ya Serikali ya kujenga Serikali mtandao
imara mfumo uliopo sasa kwenye baadhi ya taasisi humfanya mwananchi
achukue muda mrefu kupata huduma.
Ameeleza kuwa taasisi za Serikali
zinazofanya kazi katika mazingira yanayofanana zinaposhirikiana katika
kutoa huduma Kupitia Serikali mtandao mwananchi wa kawaida hatajua nini
kinaendelea, atakachokipata mwisho ni majibu ya huduma aliyoiomba kama
ni Bandarini atachukua mzigo bila usumbufu wowote kwa kuwa suala la
kodi, upakuaji na upakiaji wa mizigo na ukaguzi halitamgusa mwananchi.
Ameongeza kuwa ili Serikali
mtandao iweze kufanya kazi yake ipasavyo nchini lazima kuwe na
miundombinu ndani ya taasisi au nje pia uwepo wa mifumo Tumizi (
Application Systems) inayoshughulikia masuala mbalimbali, wafanyakazi
pamoja na Sera, miongozo na taratibu za kusimamia TEHAMA kuwezesha
huduma mtandao ( e – Servieces).
Dkt. Jabiri amesisitiza Tanzania iko
kwenye hatua ya kwanza na ya pili, kwa maana ya taasisi nyingi za
Serikali zina tovuti zenye taarifa za awali za kumsaidia mtu kujua nini
kinapatikana au kutolewa na taasisi za serikali ili aweze kuchukua hatua
ya kupata huduma.
Amesema Wakala ya Serikali
mtandao imefanikiwa kuweka mifumo kwa maana ya Tovuti kuu ya Serikali,
Tovuti ya Wananchi, Tovuti ya data huria ambayo ina taarifa mbalimbali
za wananchi kuhusu Maji, Barua pepe ya Serikali (GMS) ambayo sasa
inatumiwa na jumla ya taasisi 117 za Serikali na Balozi mbalimbali kwa
lengo kuepuka matumizi ya barua pepe za muda.
|
May 18, 2016
SERIKALI KUWAWEZESHA WANANCHI KUPATA TAARIFA NA HUDUMA MBALIMBALI KUPITIA SIMU ZAO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment