![]() |
| Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Kwa miaka mingi hapa nchini Tanzania, Kilimo
kimetajwa kuwa uti wa mgongo wa Taifa. Ikumbukwe kuwa miaka ya Sabini
za mwanzoni kuliwahi kuwepo kauli kuhusu kilimo iliyosema “Kilimo cha
Kufa na Kupona”. Kauli hii ililenga kuondoa njaa iliyokuwa inalikabili
Taifa. Kwa miaka ya hivi karibuni, serikali ikaja na Kauli Mbiu ya
“Kilimo Kwanza”. Hizi zote ni jitihada za kuinua kilimo ambacho
kinategemewa na walio wengi hapa kwetu.
Kilimo ni eneo la kipaumbele katika uchumi
wa Tanzania licha ya kuwa kilimo nchini bado kinategemea kwa kiasi
kikubwa mvua na hali ya hewa kwa ujumla .
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka ya hali ya
hewa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi zinasema mvua za
masika zimeshaanza katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua
kwa mwaka. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo machache yanatarajiwa kupata mvua
za wastani hadi chini ya wastani.
Hali ya unyevunyevu wa udongo inatarajiwa
kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo katika maeneo mengi.Hata hivyo,
mvua za juu ya wastani zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha hali
ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi hivyo kuathiri mazao na hata
kusababisha mafuriko na kuharibu mazao.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania, msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi
Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini
Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), Pwani ya Kaskazini,
(Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-Kaskazini pamoja na
Visiwa vya Unguja na Pemba), Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera,
Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa
Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa
maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya Kusini mwa ukanda huo
yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
tahadhari imetolewa kwa wakulima wote kuwa makini na mvua hizi za masika
zinazoendelea kwani zinatarajiwa kunyesha kwa wingi katika baadhi ya
maeneo kulingana na uelekeo wa upepo katika maeneo mengi ambayo
yanayopata mvua za msimu wa masika.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa na Mamlaka ya
Hali ya Hewa hivi karibuni umezingatia zaidi kipindi cha msimu(miezi
mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria
vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi
katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa
kati na mfupi.
Wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli
za kawaida za kilimo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu
za kuongeza uzalishaji, kupanda mazao na miti kuzuia mmomonyoko wa
udongo pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo katika
matumizi sahihi ya ardhi na mbegu. Hata hivyo, katika maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani,upungufu wa unyevunyevu
wa udongo unaweza kujitokea hususan katika vipindi vya kukosekana kwa
mvua. Wakulima waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa
maafisa ugani katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo Sokoine(SUA) katika tafiti zao wametoa ushauri kuhusu namna
bora ya kilimo cha baadhi ya mazao kwa kuzingatia taratibu sahihi za
kilimo za mazao hayo wakati huu wa mvua za masika.
Ushauri kuhusu mtama
Mtama unatarajiwa kukua vizuri wakati wa
masika. Wakati wa kupanda mtama, wakulima wanashauriwa kuanza
utayarishaji wa mashamba kabla ya mvua. Upandaji kavu (yaani upandaji
kabla ya mvua) unapendekezwa sana kwa mtama na ni bora wakulima wapande
katika wiki za tatu na nne za Machi. Wakulima wanaweza kuanza kupanda
mtama katika mwezi wa pili (Februari) kabla ya kupanda mimea mingine.
Katika upandaji kavu, kina cha udongo (yaani urefu wa shimo kwenda
chini) kinahitajika kuwa sentimeta tano ikilinganishwa na upandaji
unyevu (yaani upandaji wakati udongo una maji) ambapo kina kinahitajika
kuwa kama sentimita mbili nukta tano (2.5) hadi sentimita nne.
Wakulima wanashauriwa kuweka mbolea vizuri
kwa kuchanganya na udongo.Wakulima wanashauriwa pia kupalilia angalau
mara mbili wakati wa kukua kwa mimea.
Ushauri kuhusu Maharagwe
Ili kupata mazao bora ya maharage,
umwagiliaji wa maji ni muhimu. Kwa ajili ya mvua ya kawaida au nyingi
inayotarajiwa, uhifadhi wa maji ya mvua unahitajika ili maji haya
yatumike wakati wa mvua chache. Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu za
umwagiliaji wa mifereji ya juu au chini wakati wa ukavu kwa milimita 50
kwa wiki hadi mwisho wa msimu. Kwa kawaida, joto huwa haina athari mbaya
kwa maharage, kama kiwango kizuri cha maji kimo mchangani.
Ushauri kuhusu Mahindi
Wakulima wanashauriwa waanze kupanda mahindi
kabla ya mwanzo wa mvua katika wiki ya tatu au nne ya Machi. Mahindi
yanafaa kupandwa punde tu hali ya udongo na joto lake linapofaa kwani
kuchelewesha upandaji kunaweza kusababisha upungufu wa mavuno,kwa sababu
mahindi yanahitaji unyevu bora zaidi wa udongo wakati wa upandaji,
wakulima wanashauriwa kutumia hatua zinazofaa za kuhifadhi udongo.
Kutumia mbinu za ukulima bora ni pamoja na
upandaji miti na ukulima wa mseto ambao unaweza kupunguza mmomonyoko wa
udongo na kuongeza ubora wa maji na udongo. Wakulima wanahimizwa wawe na
mbinu ya kuondoa maji katika maeneo yanayopata mvua nyingi ili kuzuia
uharibifu wa mimea. Uchimbaji wa mitaro ya kuondoa maji haya unaweza
kuzuia mafuriko na pia mmomonyoko unaopoteza udongo wa juu wenye rutuba.
Kuchanganya mchanga na mbolea ya shamba kunaweza kutayarisha udongo kwa
unyonyaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa imetoa wito kwa
wakulima wote nchini kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo
ili kuondokana na usumbufu utakajitokeza katika msimu huu wa masika
unaoendela nchini.
Mamlaka ya hali ya hewa imewaomba watanzania
kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa
na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania ili kujua hali inayotarajiwa kuwepo
kwa kipindi chote hiki cha msimu wa mvua za masika.
|
May 17, 2016
WAKULIMA WAWE MAKINI NA MVUA HIZI ZA MASIKA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment