Idadi
ya mauzo katika soko la hisa Dar es salaam (DSE) imekua kwa asilimia 57
na kufikia shilingi bilioni 3.3 kutoka shilingi bilioni 2.1 wiki
iliyopita kutokana na ukubwa wa idadi ya mauzo.
Katika
taarifa iliyotolewa na Afisa Mwandamizi wa Masoko DSE Bi. Mary Kinabo
imesema kuwa idadi ya mauzo hayo yamekua kutokana na kupanda kwa idadi
za hisa zilizouzwa kutoka shilingi milioni 1.6 hadi kufikia shilingi
milioni 2.2.
Aidha
taarifa hiyo iliongeza kuwa Benki ya CRDB imeendelea kuongoza kwa idadi
ya hisa zilizouzwa na kununuliwa kwa asilimia 49 ikifuatiwa na Soko la
hisa DSE ikiwa na asilimia 43 na ya tatu ni kampuni ya Bia nchini TBL
yenye asilimia 4.
Taarifa
hiyo iliendelea kueleza kuwa ukubwa wa mtaji wa soko umepanda kwa
asilimia 0.67 na kufikia shilingi trilioni 23.4 kutoka trilioni 23.2
wiki iliyopita na ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani umebaki kwa
shilingi trilioni 8.4.
Mbali
na hayo taarifa hiyo imeeleza kwamba licha ya mauzo kupanda lakini
viashiria vya soko katika sekta ya viwanda vimeshuka kwa alama 19.47
baada ya bei za hisa kutoka TBL kushuka kwa asilimia 0.66 huku sekta ya
huduma za kibenki kupanda kwa alama 29.89 kutokana na kupanda kwa kaunta
ya DSE na NMB.
Aidha
taarifa hiyo imeeleza kuwa viashiria vya soko katika sekta ya huduma za
kibiashara wiki hii imebaki kwenye hali yake ya wiki iliyopita baada ya
bei za hisa za Swissport kubaki kwa shilingi elfu 3.543.
Na Ally Daud-Maelezo


No comments:
Post a Comment