WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) imepiga marufuku usafirishaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa
ambapo mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo
ambavyo Serikali inavihitaji, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo
wake.
Imesema
zuio hilo linakwenda sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo
ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa,
pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini
na vijijini.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema
uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya maduhuli stahiki ya
rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.
Alisema
moja ya majukumu ya TFS, ni kuhakikisha inaanzisha na kusimamia
rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na
kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni kosa kuvuna hovyo
misitu na bidhaa zake bila kibali.
Mtendaji
huyo alisema kila zao linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru
stahiki na kukatiwa risiti, hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia
mbalimbali zinazokatazwa ni kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.
“Mazao
ya misitu, ikiwemo mikaa ni kosa kuuzwa na kusafirishwa bila kuwepo
kibali na risiti. Muuza mkaa lazima uwe na risiti, na wewe mnunuzi
tukikukamata na gunia la mkaa na huna risiti utawajibika.
“Tunataka
kuhakikisha maduhuli ya mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata
matumizi endelevu ya rasilimali za misitu hivyo ni biashara hii ya miti,
mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe wazi.
“Ni
marufuku kusafirisha mazao ya misitu usiku, kama mtu ana vigezo vyote
tunavyovihitaji kusafirisha mazao ya misitu anatakiwa kusafiri kuanzia
saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni, ikipita hapo, weka pembeni gari mpaka
asubuhi,” alisema.
Aidha
alisema TFS chini ya Wizara ya Maliasili ina Meneja miti kwenye kila
wilaya, ambao wanafanya kazi kwa karibu na Maofisa Watendaji wa vijiji
ambao hushirikiana kutoa vibali kwa kuvuna miti stahiki kisheria na
kutoa risiti.
Alisema
risiti hizo pamoja na vigezo vingine ikiwemo kuwa na usajili wa TFS,
leseni ya biashara na namba ya utambulisho wa mfanyabiashara (TIN), hati
ya kusafirisha mazao ya misitu humfanya mfanyabiashara kuruhusiwa
kuendelea na biashara ya mazao ya miti nchini.
Profesa
Silayo alisema TFS wataendelea na majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni
pamoja na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, alipozungumza na watumishi wa wizara hiyo mapema mwezi
uliopita.



No comments:
Post a Comment