|
Baadhi ya waandishi
wa habari na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania na EATV wakiwa katika uzinduzi wa
tuzo za wasanii za EATV zitakafanyika Disemba 10 2016 na kuwahusisha wasanii
wote wa Afrika Mashariki.
Katika kuleta chachu ya sanaa hapa nchini kituo
cha Televisheni cha East Africa(EATV)kimeanzisha tuzo za wasanii ambazo
zitafanyika katika ukumbi wa Mlimani city mwezi Desemba .
Akiongea wakati
wa kutangaza uzinduzi wa tuzo hizo katika mkutano na waandishi wa habari,Mkuu
wa masoko wa kituo cha televisheni cha EATV,Roy Mbowe alisema kuwa tuzo hii ni
kwa ajili ya wasanii wa tasnia mbalimbali na kwa kuanzia mwaka huu itawahusu
wasanii wa tasnia ya muziki na filamu katika nchi za Afrika Mashariki.
“Pengine mnaweza mkajiuliza kwanini EATV imeamua kubeba
jukumu hili la utoaji tuzo za EATV. Kwa
wafuatiliaji wa mambo ya kimataifa
watabaini kuwa vituo mbalimbali vikubwa duniani kama kilivyo kituo cha EATV
vimekuwa vikitoa tuzo na sisi tukaona kwanini tusipende kazi za wasanii wa
kwetu kwa kuzizawadia tuzo na kuzikuza”.Alisema
Alisema utoaji wa tuzo hizi unaanza mwaka huu na hafla ya utoaji tuzo itafanyika Desema 10
na kituo bado kinaandaa mchakato mzima wa jinsi ya kushiriki kuwania
tuzo,vipengele vitakavyoshindaniwa ambavyo alidai kuwa vitatangazwa baadaye na
aliishukuru kampuni ya Vodacom kwa kutoa udhamini wa tuzo hizi zenye lengo la
kutoa motisha kwa wasanii .
Mbowe aliishukuru serikali kupitia Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) kwa kutoa kibali cha kuendesha zoezi hili ambalo linalenga
kukuza Sanaa na kuboresha maisha ya wasanii “Tunatoa shukrani kwa serikali ya
Tanzania kutuunga mkono na tutaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali
kuboresha tuzo hii”Alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Vodacom
Tanzania, Nandi Mwiyombella alisema Vodacom inafurahi kudhamini tukio hili
muhimu lenye lengo la kuwapatia motisha wasanii wa kanda ya Afrika Mashariki.
“Moja ya dhamira ya kampuni ya Vodacom ni kuibuka na kukuza
vipaji ndio maana kampuni imekuwa mstari wa mbele kudhamini michezo na Sanaa kwa kuwa inaamini kupitia
sekta ya michezo watanzania wengi mbali
na kupata burudani inawezesha kuongeza wigo wa ajira na kampuni itaendelea
kuwezesha wasanii na wanamichezo kama ambavyo hivi sasa inavyodhamini ligi ya
soka ya Vodacom Premier League na mashindano ya kucheza muziki wa dansi
yanayojulikana kama Dansi 100.
Afisa Uhusiano wa Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA),Alistides Kwizera alipongeza kituo cha EATV kwa kuanzisha wazo lenye
lengo la kukuza tasnia ya sanaa nchini na aliipongeza Vodacom kwa kudhamini
tukio hili.
“Serikali kupitia BASATA iko pamoja nanyi kwa kuwa
imedhamiria kuinua vipaji vya sanaa na kkuwawezesha wasanii kujiajiri hivyo
tutaendelea kuwaunga mkono wakati wote na natoa wito kwa wasanii kujitokeza
kuchangamkia fursa hii ambayo imejitokeza kwa ajili ya kuwatangaza na
kuwawezesha kujipatia mapato kupitia kazi zao za sanaa”.Alisema.
|
No comments:
Post a Comment