WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inalinda amani ya
nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote
kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.
“Hatuzuii
kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa
na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya
vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati
akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mkoa wa Rukwa mara
baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Alisema
Serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi
zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha
amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa
kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.
“Suala
la uhamasishaji wananchi juu ya utunzaji wa amani ni la lazima hivyo
viongozi wa dini na wazee kwa pamoja tushirikiane katika kukemea vitendo
vya uchochezi kwasababu vurugu zikitokea Watanzania hatuna mahali pa
kukimbilia,” alisema.
Aidha,
Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja
na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na inachangamoto
nyingi.Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha
uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.
Awali,
Sheikh wa mkoa wa Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali amesema madhehebu ya
dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila anahofu na viongozi wa vyama
vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.
Kufuatia
hali hiyo Sheikh Akilimali aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani
kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo
kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Sheikh
Akilimali alisema kwa sasa wananchi wako huru kwenda kufanya ibada
misikiti na makanisani kutokana na uwepo wa amani, hivyo aliwasisitiza
wanasiasa kutothubutu kuichezea amani.
“Tafadhalini
wanasiasa msituharibie amani ya nchi yetu. Amani haichezewi tunaona kwa
wenzetu wanavyohangaika, wanaishi kwa tabu sisi hatujazoea kukimbia.
Sisi Watanzania ni moja na tunaishi kwenye nyumba moja hivyo hatuna budi
kushirikiana kuilinda amani yetu,” alisema.
Kwa
upande Katibu wa Wazee mkoani Rukwa, Kanali Mstaafu, John Mzurikwao
alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia kutatua kero mbalimbali
zinazoukabili mkoa huo zikiwemo za malipo ya pembejeo kwa mawakala wa
kilimo pamoja na mgogoro wa ardhi katika shamba ya Efatha.
Waziri
Mkuu alisema suala la malipo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo
linafanyiwa kazi na watalipwa baada ya Serikali kukamisha zoezi la
uhakiki wa madeni hayo ili kujiridhisha kama kweli wakulima wapatiwa
pembejeo na kwa kiwango gani.
No comments:
Post a Comment