KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 26, 2016

AGIZO LA MKUU WA MKOA GAMBO LATEKELEZWA ARUSHA

daqaro
Mkuu wa wilaya ya  Arusha,Gabriel Daqarro
……………………………………………………………
 Na Mahmoud Ahmad Arusha,
Hatimaye halmashauri ya jiji la Arusha imetekeleza agizo lililotolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo  la kulipa madeni yote ya walimu wa shule za msingi  na sekondari jijini Arusha ambapo jumla ya sh, 169  milioni zimelipwa kwa ajili ya walimu hao.
 
Fedha hizo ni zile ambazo zilikuwa ni madeni ya walimu waliyokuwa wakidai kwa muda mrefu katika Jiji la  Arusha zimelipwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha alilolitoa hivi karibuni.
Gambo, alipokutana na walimu wa shule za msingi na sekondari Mkoani Arusha alipokea  malalamiko mengi  moja ya malalamiko ni madai sugu ya walimu na ndipo alipoiagiza halmashauri  zote na jiji Mkoani Arusha kulipa madeni hayo ndani ya siku 14. Katika kutekeleza maagizo hayo,Mkuu wa wilaya ya  Arusha,Gabriel Daqarro alisema Jiji limetekeleza ndani ya siku mbili na kufanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kwa walimu wote wa msingi na sekondari.
 
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini hapa Daqarro alisema Jiji la Arusha lina jumla ya walimu 701wa msingi na sekondari na madai hayo yalikuwa ya kipindi cha mwaka 2015/16 ambapo walikuwa wakidai kiasi cha sh,16 milioni na Sasa  wamelipwa fedha zote na kwamba hakuna madai yoyote.
 
 Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inawajali na kuwalinda walimu wote na kuwapa stahili zao za msingi kwa wakati bila ya kipingamizi chochote.
 
 Mkuu huyo alisema walimu walikuwa wakidai stahilizao za muda mrefu ikiwa ni pamoja na fedha za kujikimu,likizo,nauli,matibabu na upandishwaji madaraka na  fedhahizo zote wamelipwa.
 
Alisema kwa sasa serikali ya wilaya ya Arusha inataka kuona walimu wakifanya majukumu yao ya msingi katika kupandisha elimu ikiwa ni pamoja na kufundisha wanafunzi bila  ya kuwa na msongo wa mawazo.
Akizungumzia upatikanaji wa fedha hizo kwa muda huo mfupi alisema Halmashauri ya Jiji la Arusha iliamua kusitisha malipo yasiyokuwa ya lazima na kuondoa malipo ambayo yalikuwa kinyume na taratibu zikiwemo posho za madiwani  na ndio maana fedha hizo zimepatikana.
 
Mkuu wa wilaya  alisema sio kwamba fedha za kuwalipa walimu zilikuwa hazipo bali zilikuwa zikilipa vitu vilivyo nje ya utaratibu na kutokana na usimamizi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Athumani Kihamia ameweza kubana mianya yote ya ulaji fedha hizo.
  
 ‘’Fedha nyingi za Jiji la Arusha zilikuwa zikilipwa kiholela holela na kufanya walimu kuteseka nakuumia pasipokuwa na sababu za msingi’’  Kwa sasa mianya hiyo imezibwa na ndio maana sasa fedha zinaonekana na zinalipa wahusika wenye kudai madeni yao ya muhimu kama haya ya walimu’’alisema Daqarro

 Alisema kwamba wapinzani hususani Chadema wamekuwa  wakitumia madai ya walimu nchini kama hoja ya msingi na sasa serikali imeamua kutekeleza madai hayo wanaanza kubeza.
 
Alisisitiza kwamba madiwani wa Chadema jijini Arusha waliamua kujiongezea posho kutoka sh,60,000 hadi 80,000 kinyume na utaratibu na kuhusu hoja kwamba walikuta posho hizo kabla ya kuingia madarakani haina mashiko.
 
 “Hawa wamejiongezea posho kutoka sh,60,000 hadi 80,000 kinyume na utaratibu na wanasema kwamba  wamezikuta hizi posho kwanini miezi minane waliyoingia wasizifute kama ziko kinyume?”alisema Daqarro
 
Hata hivyo,alisema kwamba ni jambo la ajabu kuona diwani wa kata ya Kaloleni iliyopo katikati ya mji akilipwa sh,80,000 kama posho ya nauli ilhali mtu akisafiri kutoka Dar es salaam hadi Arusha analipa nauli kiasi cha sh,30,0000.

No comments:

Post a Comment