Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa inatumia fursa hii kufafanua kwamba, msimamo alioutoa Msajili wa
Vyama vya Siasa kuhusu mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF una maana
kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa kwake na pande mbili
zinazosigana na kwa mujibu wa Katiba ya CUF toleo la 2014, Msajili
alijiridhisha kwamba, Profesa Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa
wa chama cha CUF, kwa sababu alitengua barua yake ya kujiuzulu kabla
haijakubaliwa na mamlaka yake ya uteuzi, kama inavyoelekeza ibara ya
117(2).
Aidha, Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa inaviasa vyombo vya habari kufanya jitihada za kuelewa msimamo
wa Msajili wa Vyama vya Siasa, badala ya kuandika habari au makala
zinazopotosha umma.
Hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa inatumia fursa hii pia, kukanusha taarifa zinazoenezwa katika
vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kwamba, Msajili wa Vyama
vya Siasa amesema kuwa, hakumrudishia Profesa Lipumba Uenyekiti wa Taifa
wa CUF, bali Profesa Lipumba kajirudisha mwenyewe kinyemela. Habari
hiyo siyo ya kweli, imepotoshwa kwa makusudi, Watanzania wanapaswa
kuipuuza.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa inawaasa viongozi wa kitaifa wa chama cha CUF, kusoma kwa makini
msimamo uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa na kuuheshimu, kwani
kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, Msajili wa Vyama
vya Siasa anao wajibu wa kujiridhisha kwamba, mabadiliko yoyote
yaliyofanywa katika uongozi wa taifa wa chama cha siasa, ni halali na
yamefanywa na mamlaka halali kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama
husika.
Sisty L. Nyahoza
Kny: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
No comments:
Post a Comment