KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

October 5, 2016

CUF SASA KUFIKISHANA MAHAKAMANI

prof-lipumbaKufuatia mgogoro uliopo katika Chama cha Wananchi (CUF) baina ya uongozi wa chama hicho na Profesa Ibrahim Lipumba waliyemfuta uanachama, viongozi wa CUF wamepanga kwenda mahakamani ili wapate suluhu ya kisheria.
Jopo la Mawakili wa CUF wakiongozwa na Mwanasheria Tundu Lissu linataraji kufungua mashitaka mahakamani dhidi ya Lipumba na kundi lake wiki ijayo.
Kwa madai kuwa Lipumba amevamia ofisi za chama hicho na kuikalia kinyume cha sheria pamoja na kuharibu baadhi ya mali za chama hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro wakati akizungumza na mtandao wa MO BLOG kwa njia ya simu, amesema mawakili hao watakutana siku ya Ijumaa au Jumamosi ili kuandaa mashitaka na kwamba yatafunguliwa rasmi mahakamani kuanzia wiki ijayo.
“Mawakili watakutana Ijumaa hii au Jumamosi ili wiki ijayo waanze kufanya hiyo kazi ya mahakamani,” amesema Mtatiro.
Hata hivyo, Bodi ya Wadhamini ya CUF hapo jana ilitoa tamko la kutaka kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Lipumba ili alipe gharama za hasara, ilizodai kuwa Lipumba alizisababisha baada ya kuvamia Mkutano Maalumu wa Taifa wa CUF uliovurugika Agosti 21, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl , Ubungo Plaza.
Bodi hiyo ilidai kuwa hasara iliyosababishwa na Lipumba kwa kuvuruga mkutano huo ni Milioni 600, na takribani milioni 50 kwa kuvamia ofisi ya chama hicho iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam na kufanya uharibifu wa mali za chama hicho zenye thamani ya fedha hiyo.
Bodi hiyo ilisema itachukua hatua za kisheria zaidi kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kurejesha chini ya himaya yake, mali za chama ikiwemo jengo la ofisi ya chama hicho kutoka mikononi mwa Lipumba.
Aidha, baada ya bodi hiyo ya wadhamini kutoa tamko la kumshitaki na kutomtambua Prof. Lipumba. Upande wa Lipumba ulidai kuwa bodi hiyo haina baraka na mamlaka ya kuamua jambo lolote juu ya Lipumba.
Abdul Kambaya, aliye karibu na Lipumba ameuambia mtandao wa Modewjiblog.com kuwa maamuzi ya kikao cha bodi hiyo hayakuwa halali kwa kuwa akidi ya wajumbe halali haikutimia.
Ndipo mtandao huu ulipomuhoji Mtatiro zaidi juu ya ufafanuzi wa malalamiko hayo.
Mtatiro amefafanua kuwa, kikao cha bodi ya wadhamini kilichoketi juzi, kilikaliwa na wajumbe halali 6, na kwamba wajumbe 3 hawakuhudhuria, ambapo wawili ni wafuasi wa Lipumba wakati 1 hakuhudhuria kutokana na kupata udhuru ya safari kwa siku hiyo.
“Idadi ya wajumbe wa bodi ya wadhamini iko 9, waliofanya kikao 6 akidi hii ni halali na angekuwepo yule mmoja aliyepata dharura ya safari wangekuwa saba, Lipumba amebaki na wajumbe wa bodi wawili tu,” amesema.
Mtatiro amesema maamuzi yoyote yatakayotolewa na bodi hiyo ni halali kwa kuwa akidi ya wajumbe wake ingawa pungufu lakini inatambulika na kuruhusiwa kisheria.
Pia kumekuwepo na tuhuma kutoka upande wa Lipumba kuwa miongoni mwa sababu ya mgogoro wa chama hicho, ni masilahi binafsi baina ya upande wa Zanzibar na Bara kwa madai kuwa Zanzibar inanufaika na ruzuku za chama hicho kuliko Bara.
Mtatiro amefafanua kuwa, upande wa Bara ndio unaofaidi ruzuku za chama hicho kuliko Zanzibar na kusema kuwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF linatoa asilimia 70 ya ruzuku ya chama hicho Bara kwa kuwa ina wilaya nyingi za kichama.
Na kwamba Zanzibar inapokea ruzuku ndogo ya asilimia 30 kwa sababu ina idadi ndogo za wilaya

No comments:

Post a Comment