Sehemu ya Chanzo cha maji cha Mto
Mbukwa ambacho Kampuni ya TANWAT imepanda miti ndani ya mita sitini na
kutishia uhai wa chanzo hicho. Kampuni hiyo imeamriwa kuondoa miti hiyo
mara moja na kutakiwa kulipa faini ya Shilingi Milioni Hamsini.
Bustani darasa ya mbogamboga
maarufu kwa jina la ‘vinyungu’ inayozingatia uhifadhi wa mazingira kwa
kutolimwa pembezoni mwa chanzo cha maji.
Wakazi wa Kijiji cha Owadi Maheve
ambao wanajishughulisha na kilimo cha mbogamboga kwa kufuata utaratibu
wa kutolima kwenye vyanzo vya maji. Waziri Makamba amechangia mifuko
hamsini ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika
kufundishia njia bora zaidi za kilimo.
Chanzo cha maji cha Mtitafu
kilichopo Kata ya Igima, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe
kilichohifadhiwa vizuri na kuwa mfano mzuri wa kuigwa.
……………………………………………………………………..
Na Lulu Mussa
Njombe
Wadau wa Mazingira wametakiwa
kufuata Sera, Kanuni na Tararibu katika kuendesha shughuli zao. Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January
Makamba ameyasema hayo leo Mkoani Njombe alipokuwa katika mwendelezo wa
ziara ya kutembelea Mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kujionea
hali ya mazingira na kutoa maelekezo stahiki.
Waziri Makamba ametoza faini
Kampuni ya TANMAT kwa kuikuka Sheria ya Mazingira inayokataza upandaji
wa miti ndani mita sitini kutoka katika chanzo cha maji. “Kampuni hii
imevunja sheria hivyo hamna budi kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe mfano
na kwa wengine” alisisitiza Waziri Makamba.
Kampuni hiyo imeagizwa kulipa
faini hiyo ndani siku saba na endapo watakiuka hatua kali zaidi za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Waziri Makamba pia ameiagiza Kampuni
hiyo kuondoa miti hiyo ambayo si rafiki kwa mazingira mapema
iwezekanavyo na kuagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kuwapa ‘Restoration Order” kurudisha mazingira katika
hali yake ya kawaida.
Katika hatua nyingine, Meneja wa
Kampuni hiyo inayojishughulisha na upandaji wa miti Bw. Joseph Shirima
amekiri kupokea barua zizoelekeza kusitisha uharibifu huo wa Mazingira
katika chanzo cha Mto Mbukwa ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wengi
wa Wilaya ya Wanging’ombe.
Aidha, Waziri Makamba ameupongeza
Uongozi wa Mkoa wa Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi
kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachi kuacha kulima bustani za
mbogamboga pembezoni mwa mito.
Dkt. Nchimbi alimfahamisha kuwa
kwa sasa kuna kikundi kijulikanacho kwa jina la “Jerusalemu” kinachotoa
mafunzo kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha
uhifadhi wa mazingira ambapo lengo ni kuanzisha vituo kama hivyo vya
mafunzo kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Waziri Makamba alitembelea na
kuona “vinyungu” ambavyo awali vilikua vikilimwa kando ya mito na
kwasasa vimehamishiwa majumbani, katika kuunga mkono jitihada hizo njema
Waziri Makamba amechangia mifuko Hamsini ya Saruji kwa ajili ya ujenzi
wa darasa litakalotumika kutoa mafunzo zaidi ya kilimo.
Waziri Makamba Waziri Makamba
anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini,
hii leo amewasili katika Mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment