Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilaya ya Mkalama mkoa wa
Singida,umetumia zaidi ya shilingi Milioni 206.2 kulipa kaya masikini
5,901, ili kuzinusuru na makali ya maisha, kati ya Septemba mwaka huu
hadi sasa.
Akizungumza na waandishi wa
habari juzi,mratibu wa TASAF wilaya ya Mkalama, Athumani Dulle, alisema
malipo hayo yameelekezwa katika sekta ya afya na elimu.“Mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya TASAF 111, unawezesha kaya zenye hali duni katika kupata lishe bora,huduma za afya na za elimu. Hapa walengwa mahususi ndani ya kaya hizi, ni watoto wenye umri chini ya mitano, watoto wanaosoma shule za awali, msingi na sekondari.Pia wajawazito,” Dulle alifafanua.
Akifafanua zaidi, alisema lengo la ruzuku ya sekta ya elimu kwa kaya masikini ni kuboresha mahudhurio ya wanafunzi shuleni.
“Siku ya malipo mahudhurio shuleni ya walengwa yanakaguliwa,endapo yatakuwa sio mazuri,na malipo pia hayatakuwa mazuri,yatapunguzwa.Pia mahudhurio ya watoto ambao wanapewa ruzuku ya afya,mahudhurio yao kliniki nayo yatakaguliwa,” alisema.
Kuhusu ruzuku ya afya, Dulle alisema walengwa wa ruzuku hiyo, ni watoto wa umri chini ya miaka miwli hadi mitano ambao ruzuku hiyo itasaidia wapelekwe kwenye vituo vya afya na zahanati.
Katika hatu nyingine, mratibu huyo alisema kaya zilizoandikishwa kwenye mpango wa TASAF 111, zimeongezewa fursa nyingine ya kujiongezea kipato, nayo ni ajira za muda mfupi.
“Kwa mfano walengwa wa kijiji hiki hapa cha Nkinto,wao wameibua mradi wa ujenzi wa bwawa la maji kwa ajili ya kupata maji kwa matumizi ya nyumbani,kilimo cha bustani na kunyweshea mifogo,kwa umbali mfupi.Katika ujenzi huu,kila kaya inalipwa ujira kwa siku 15 kila mwezi kwa muda wa miezi minne”,alisema mratibu huyo.
Kwa upande wa walengwa,kwa ujumla wao wameishukuru serikali na wafadhili wa mpango wa TASAF 111, kwa madai kwamba ruzuku wanazopata, zimewapunguzia makali ya maisha, wameweza kujenga nyumba bora na vile vile, wameanzisha ufugaji wa kuku na mbuzi, kwa ajili ya kuiongezea kipato.
Eliwaza Ngimba,alisema kupitia ruzuku anayopata kutoka TASAF, ameweza kununua mbuzi watano ambao amedai hata TASAF ikisitiza mpango wake, ana uhakika mbuzi hao watakuwa wanamwingizia kipato. Pia ameifanyia ukarabati nyumba yake ndogo, kwa kuiezeka kwa bati.
Naye munufaikaji mwingine wa TASAF 111, mhandisi Paulo Ntoga, alisema baada ya wao kuondokana na mawazo potofu kwamba fedha hizo za ruzuku ni za freemason, sasa wamezikubali na wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Mimi niwaase tu wanufaikaji wenzangu,tutumie ruzuku hizi vizuri kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.Tukifanya hivyo,pia tutakuwa tumeivutia serikali na wafadhili kuboresha mpango huu kwa kuongeza kiwango cha malipo na mradi wenye uwe endelevu,” alisema mhandisi Paulo.
Na Nathaniel Limu, Mkalama


No comments:
Post a Comment