Benny Mwaipaja, MoFP-Washington DC, Marekani
MAWAZIRI
wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali za kiafrika,
wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF,
wamekutana Jijini Washington DC, Marekan,i na kuzitaka Taasisi hizo
kuweka mipango inayoakisi na kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo
ikiwemo, uhalifu, umasikini, mizozo ya kivita na majanga yanayotokana
na mabadiliko ya tabia nchi
Aidha,
Viongozi hao wamezitaka taasisi hizo kuweka uwiano wa uwakilishi wa
uongozi wa juu ili kuhakikisha kuwa maslahi mapana ya nchi hizo
yanalindwa na maendeleo endelevu yanafikiwa kwa haraka.
Akizungumza
kwenye moja ya mikutano hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, ambaye kiutaratibu ni mmoja wa Magavana wa Benki ya Dunia na
IMF, amesema kuwa mashirika hayo ya fedha ya kimataifa yanamchango
mkubwa kwa maendeleo ya nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania.
Hata
hivyo amesema kuwa mdororo wa uchumi duniani, ambao unaonesha kuwa
viwango vya ukuaji wa uchumi vilivyokadiriwa kufikiwa kwa asilimia 3,
havitafikiwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wake hivi sasa ni
asilimia 1.5 tu, unaashiria namna nchi wanachama zinatakiwa kujipanga
kuhakikisha kuwa uchumi unapanda.
Dkt.
Mpango amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kwa wastani wa
asilimia 7 kwa mwaka lakini changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha kuwa
uchumi huo unaonekana katika maisha ya kawaida ya wananchi wake
“Kila
mara utasikia malalamiko ya wananchi kwamba uchumi wetu unakua kwa namba
tu hawaoni ni kwa kiasi gani uchumi huo wanauona katika maisha yao ya
kawaida kwa hiyo ili uchumi uhesabike kuwa unakua ni lazima uwe jumuishi
na ushirikishe watu wengi” alisema Dkt. Mpango
Amesema
kuwa hali hiyo itawezekana ikiwa sekta zinazochangia maendeleo kwa kasi
zaidi kama kilimo, uvuvi, biashara ya miamala ya simu, miundombinu na
viwanda, zitaimarishwa ili kukuza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
“Tunataka
kilimo kiwe cha kisasa na cha kibiashara kwa kutumia zana na pembejeo
bora za kilimo, uongezaji wa thamani ya mazao na kuwa na masoko ya
uhakika ili kukuza ajira nyingi hususani kwa vijana” Aliongeza Dkt.
Mpango
Amebainisha
kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati yake na Benki ya
Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF na kuwataka watanzania waelewe
kuwa mikopo na ruzuku zinazotafutwa na serikali yao ni kwaajili ya
kuwaletea maendeleo kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija.
Wajumbe
wa Tanzania waliohudhuria mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha
Duniani-IMF, wakimsikiliza kwa makini Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim
Yong Kim (hayupo pichani) wakati Mawaziri wa Fedha na makatibu wakuu
(Magavana) kutoka nchi wanachama wa Taasisi hizo kutoka Bara la Afrika,
walipokutana kama kamati, Jijini Washington DC, Marekani.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Dotto James, wakifuatilia kwa makini mkutano wa Magavana wa
Benki ya Dunia kutoka Barani Afrika uliohudhuriwa na Rais wa Benki ya
Dunia Dkt. Jim Yong Kim, Jijini Washington DC, Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Fedha wa Swaziland kushoto kwake walipokuwa kwenye mkutano na Mkurugenzi Mtendaji Bi. Christine Lagarde Jijini washington DC- Marekani


No comments:
Post a Comment