Miezi sita baada ya aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM, Paul James (PJ) (Wa pili kushoto) na mwenzake Gerard Hando kuondoka Clouds Fm na kuamia E Fm, mmoja wa watangazaji hao, PJ amerejea Clouds Fm.
PJ ametangazwa kurejea Clouds Fm na mtangazaji wa kipindi cha XXL, B Dozen akianza kwa kukumbushia jinsi PJ alivyokuwa akisoma magazeti katika kipindi cha Power Breakfast na baada ya hapo kumkaribisha kuzungumza.
Baada ya kumtambulisha PJ alitumia fursa hiyo kuelezea jinsi safari yake ya maisha ya kazi baada ya kuondoka Clouds Fm ilivyokuwa na kuwashauri wenzake kuwa inabidi kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko nchini.
“Hii ni nchi yetu lazima tuijenge pamoja, lazima utambue thamani yako, umesaidia nchi kitu gani, tujitahidi kufanya kitu chenye faida, inabidi kutumia heshima na hekima kufanya kazi yako,
“Tuna rais mzuri ana ndoto nyingi kwa ajili ya kuisaidia nchi sasa tufanye kazi kumsaidia kazi rais wetu kazi ili afanikiwe kufanya kile alichopanga kukifanya,” alisema PJ.
Aidha PJ hajataja kwa sasa atakuwa anatangaza kipindi gani kati ya kipindi alichokuwepo awali cha Power Breakfast au kipindi cha Jahazi baada ya B Dozen kumuuliza ili wasikilizaji wajue watamsikia muda gani akitangaza.