Mwanamuziki wa kike kutoka nchini Marekani, Toni Braxton amefikishwa hospitalini kwa kusumbuliwa na ugonjwa wa mfumo wa kinga wa mwili (Lupus), baada ya kuzidiwa wakati akiwa katika maandalizi ya kufanya onyesho mjini Cleveland, Marekani.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia ukurasa wake wa Twitter, ilieeleza kuwa msanii huyo hali yake ya kiafya ilibadilika ghafla hivyo ikabidi afikishwe hospitali na kwa watu wote ambao tayari walikuwa wameshanunua tiketi wazitunze kwani watatangaziwa tarehe nyingine ya onyesho.
“Toni Braxton yupo hospitali mjini Cleveland baada ya kulalamika kusumbuliwa na lupus. Kwa bahati mbaya onyesho lake la usiku Cleveland limesimamishwa,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza.
“Lupus inahitaji kufuatiliwa kwa umakini kwa muda na hili haliwezi kusababisha kusimamishwa kwa ziara yote, tiketi kwa ajili ya onyesho la leo zitunzwe na ratiba ya tarehe nyingine itatajwa haraka iwezekanavyo”
Toni alifahamika kuwa na ugonjwa wa Lupus mwaka 2011 na kwa mwezi Oktoba pekee ameshafikishwa hospitalini mara mbili baada ya hali ya kiafya kuwa mbaya hivyo kutakiwa kupatiwa huduma ya haraka.