
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo
katikati akizungumza na waandishi wa habari wakati alipokuwa
akitangaza makusanyo ya kodi ya mwezi wa tisa pamoja na uhakiki wa TIN
za wafanyabiashara ambapo amesema siku ya mwisho kwa Dar es salaam
itakuwa Oktoba 15 2016, kulia ni Gabriel Mwangosi Meneja wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa kodi TRA na kushoto ni Julius Ciza Afisa Mkuu wa Huduma
na Elimu ya Mlipa KodiTRA Makao Mkuu.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo akifafanua jambo kwa waandshi wa habari wakati wa mkutano huo uliofanyika Makao Mkuu ya TRA. Kulia ni Gabriel Mwangosi Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
……………………………………………………………………………………
Zikiwa zimebaki siku tisa
kumaliza zoezi la uhakiki na uboreshaji wa taarifa za Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa mikoa ya kodi ya Dar es salaam na
Zanzibar, tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imehakiki na kutoa
vyeti vipya vya TIN 15,467.
Zoezi la ukakiki na uboreshaji wa
taarifa za TIN linaendelea hadi tarehe 15 Oktoba 2016 katika ofisi
zilizoanishwa hivyo wananchi wenye TIN wanashauriwa kuhakiki TIN zao
kabla muda uliowekwa haujaisha kwani baada ya muda huo kuisha TIN ambayo
itakuwa haijahakikiwa itaondolewa katika mfumo wa TIN wa TRA.
Vituo vya uhakiki:
- Mkoa wa Kodi Ilala: Jengo la Mariam Tower (Shaurimoyo) na 14Rays (Kariakoo-Gerezani)
- Mkoa wa Kodi Kinondoni: Jengo la LAPF (Kijitonyama) na Kibo Complex (Tegeta) na ofisi za TRA Kimara
- Mkoa wa Kodi Temeke: Uwanja wa Taifa na Ofisi za TRA Mbagala- Zakhemu
- Wilaya ya Kigamboni – Ofisi za TRA Kigamboni
Pamoja na kuwakumbusha wananchi
kuendelea kuhakiki na kuboresha taarifa za TIN, tungependa pia
kuwakumbusha na kuwahimiza wafanyabiashara na wananchi mambo yafuatayo:-
Wasafirishaji wa mizigo kwenda mikoani
wanahimizwa kudai risiti za EFDs pindi wanaponunua bidhaa na kuwa nazo
wakati wanasafirisha mizigo ili kuepuka usumbufu pale wanapohitajika
kuonyesha risiti hizo.
Aidha wafanyabiashara nao wanahimizwa kutoa risiti kwa wateja wao ili kuhakikisha makusanyo ya kodi yanakusanywa kwa usahihi
Waagizaji wa mizigo nje ya nchi
kwa upande wao wanatakiwa kutumia mfumo wa forodha wa TANCIS kila mara
kufuatilia taarifa za upakuaji wa bidhaa zao ili kuepuka udanganyifu wa
aina yoyote.
Kwa kutumia TANCIS mzigo unaweza
kufualiwa kwa: kuandika namba ya TANSAD sehemu ya meseji/ujumbe bila
kuacha nafasi. Mfano TZDL15XXXXXX kisha tuma kwenda namba 15111. Utapata
ujumbe kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuondosha mzigo.
Kwa wale wanaoagiza magari
wanashauriwa kupata taarifa za kodi wanayostahili kulipa kabla magari
hayajafika ili kuepuka malalamiko ya aina yoyote pale matarajio yao
yanapotofautiana na makadirio ya kodi wanayostahili kulipa. Taarifa za
kodi ya magari zinapatikana katika kikokotozi kilichopo katika tovuti ya
TRA
Wale Walipakodi ambao wana madeni
mbalimbali ya kodi tunawashauri waonane na mameneja wa Wilaya au Mikoa
ya Kodi ili kuona jinsi ya kulipa madeni hayo kuliko kukaa kimya na
hivyo deni kuendelea kuongezeka.
Katika hatua nyingine TRA
imekusanya jumla shilingi trilioni 3.59 katika kipindi cha miezi mitatu
ya mwanzo wa mwaka wa fedha 2016/17 kati ya lengo la mwaka la kukusanya
shilingi trililioni 15.1 mwaka 2016/17. Makusanyo hayo yanajumuisha
mwezi Julai shilingi Trilioni 1.05, mwezi Agosti Trilioni 1.13 na
Septemba 2016 shilingi Trilioni 1.37.
Ukusanyaji wa mapato ya serikali
unaenda sambamba na kuelimisha wananchi kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi
sahihi na kwa wakati hivyo tunawaomba waandishi wa habari kuendelea
kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vyao vya habari.
Mwisho napenda kuwasisitiza waandishi wa habari kuwania tuzo ya ‘Uandishi wa Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali’
katika tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari 2016, ambazo hutolewa
na Baraza la Habari Tanzania (MCT), pale MCT itakapozindua uwasilishwaji
wa kazi za waandishi. ili kuendelea kuelimisha masuala mbalimbali
yahusuyo kodi na kujishindia zawadi mbalimbali zitakazotolewa.
‘Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard M. Kayombo
Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi


No comments:
Post a Comment