
Na. Catherine Sungura,WAMJW -Kigoma
Wakurugenzi
wa Halmashauri na wale wa hospitali za umma nchini wamepewa siku sitini
kuanzia jana wawe wamewalipa posho za wauguzi za kununua sare za kazi
ya shilingi laki moja na elfu ishirini pamoja na malimbikizo ya sare
hizo.
Agizo
hilo limetolewa mkoani hapa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia
,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 44
wa wauguzi Tanzania.
Waziri
Ummy alisema asilimia themanini ya kazi zote kwenye sekta ya afya
nchini zinafanywa na wauguzi,hivyo aliwataka wakurugenzi kuzingatia
miongozo iliyopo ya Serikali, “kama mwongozo ni kulipa elfu thelatini
lipa thelathini si vinginevyo. Serikali imekwishatoa waraka wa kazi za
ziada yaani “extra duty circular” ambao unapaswa kufuatwa hata
mnapofanya kazi usiku kwani kuna masaa ya ziada”.
“Nawaagiza
waajiri wote kuzingatia nyaraka hizi ili kuondoa malalamiko yasiyo ya
lazima, Hili ni suala muhimu kwani mnakuwa kazini siku tano hadi sita
kwa wiki hivyo mnahitaji sare walau tano ili muweze kubadilisha kila
mara. Serikali itatoa waraka wa si chini ya laki tatu kulingana na hali
ya uchumi itavyokuwa. Natumaini waraka huu utatoka mapema na kuanza
kutumika mwaka ujao wa fedha hivyo kwa mwaka huu tuendelee kutumia
waraka uliopo.
Aidha,
aliagiza baada ya siku sitini alizotoa kupatiwa orodha za halmashauri
ambazo hazitokuwa zimewalipa posho hizo na mikoa ipi”kwani kuna wauguzi
wangapi hadi mshindwe kuwapa posho za sare ,mnataka wauguzi hawa waje
kazini wawe wamevaa nini?aliuliza Waziri
Akijibu
tatizo la kusimamishwa na kufukuzwa kazi kwa wauguzi na wakunga alisema
,suala la kusimamisha au kumwachisha kazi mtumishi lina taratibu zake
ambazo zinapaswa kufuatwa. “Napenda kuliagiza Baraza la Wauguzi na
Wakunga Tanzania kuwaelimisha waajiri kuhusu hatua za kufuata katika
kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi ili yaweze kusikilizwa
kwa utaratibu zilizopo bila ya kuwaonea pande zote, Ni kweli kuwa
unapoadhibiwa bila kosa inavunja moyo, Naomba ieleweke kuwa sio nia ya
Serikali kuwaumiza wauguzi bali lengo letu kubwa ni kuondoa kero za
wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia watumishi wote wazembe na
wasiofuata maadili ya kazi”.


No comments:
Post a Comment