
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Nachingwea, Bw. Bakari Mohammed kuhakikisha hospitali ya wilaya hiyo
inakusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili,
Oktoba 16, 2016) wakati alipotembelea hospitali ya wilaya ya Nachingwea
akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amesema Serikali
ilishaagiza taasisi zote za umma kutumia mfumo wa kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha
za umma.
Amesema taasisi ambazo tayari
ziameanza kutumia mfuko huo katika ukusanyaji wa mapato zimeweza
kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. 300,000 hadi milioni nne kwa
siku.
Pia aliwaagiza viongozi wa wilaya
hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya
Jamii (CHF) ambao utawawezesha kupata huduma ya matibabu bure katika
kipindi cha mwaka mzima.
Akizungumzia kuhusu matibabu kwa
wazee, Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Mohammed kuhakikisha anafungua dirisha
la kuwahudumia wazee ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma
wanapofika hospitalini hapo.
“Mkurugenzi hakikisha watendaji
wako wa kata na vijiji wamebaini wazee wote katika maeneo yao na
kuwatengenezea vitambulisho vitakavyowawezesha kupatibiwa bure,”
amesema.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya hiyo
Dk. Samwel Laizer amesema muamko mdogo wa jamii kujiunga na CHF ni moja
kati ya changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma za afya.
Dk. Laizer amasema kati ya kaya 30,000 zilizoko wilayani Nachingwea ni kaya 7,133 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa CHF.
Awali Waziri Mkuu alizungumza na
watumishi wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa Chuo Cha Walimu na kuwataka
wabadilike ili waweze kuwatumikia wananchi kwa uadilifu bila ya kujali
itikadi zao za kidini na kisiasa.
Amesema Serikali haitamvumilia
mtumishi yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwatumikia
wananchi. “Serikali haitaridhika kuona wananchi wakizagaa kwenye ofisi
za halmashauri hiyo bila ya kusikilizwa,” amesema.


No comments:
Post a Comment